Wednesday, November 25, 2015

Ifahamu Aina Ya Mbegu Unayoipanda.


Habari ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya. Na unaendelea kupambana vikali katika shughuli zako ili tu kuhakikisha kwamba unajiletea mafanikio makubwa. Nami nakuambia vizuri pia nakusihi endelea kupambana mpaka pale utakapo timiza malengo yako. Kama kawaida kila tunapokutana hapa huwa tunakutana kwa lengo moja tu nalo ni kupeana maarifa mapya. Leo jambo nalo taka kukushirikisha ni kuhusiana na upandaji wa mbegu.
Naposema upandaji wa mbegu najua kuna wale ambao mawazo yao yatawatuma kuwa nataka kutoa darasa juu ya upandaji wa mbegu za aina fulani shambani, na kuna wale ambao watabaki na mshanga kuwa namaanisha nini haswa. Usiwe na haraka ndugu msomaji bali endelea kuisoma makala hii kisha utanielewa ni mbegu gani namaanisha. Binadamu tumekuwa wapanda mbegu wakubwa sana tena sana maana hakuna siku ambayo inapita bila sisi kupanda mbegu hizi. Lakini tofauti ya mbegu hii na ile ya zile mbegu tulizozoea kupanda mashambani sio kubwa sana ila utofauti upo tu katika mahali pa kupandia. Yaani zile mbegu za shambani tunazipanda shambani au kuzifukia ardhini. Lakini hii mbegu nayo kuletea ni mbegu inayopandwa katika ubongo wa mwanadamu yaani kichwani au akilini mwa binadamu. Nisikuache nyuma ndugu msomaji wa makala hii utakapo kuwa unasoma makala hii na kukuta neno mbegu jua neno hili linasimama au nimelitumia badala ya neno fikira. Hivyo naposema unapanda mbegu gani namaanisha kuwa unajijengea fikira gani? Nadhani mpaka hapo utakuwa umeanza kunipata sasa. Sasa mbegu tunazopamba zimegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni kama ifuatavyo:-
Mbegu mbovu, /fikira mbovu (hasi), neno mbovu si neno geni kwako ndugu msomaji lakini japokuwa unaielewa maana yake lakini mimi nataka kuielezea au kulielezea neno mbovu zaidi kwako. Tunaposema kuwa kitu Fulani ni kibovu, kwa tafsiri ya haraka haraka ni kuwa tunamaanisha kuwa kitu hicho hakifai kwa matumizi. Na kama hakifai kwa matumizi maana yake ni kuwa haupaswi kukitumia kabisa kwa namna yoyote. Na pindi ukikitumia basi chaweza kukuletea madhara makubwa sana hebu chukulia mfano wa madhara ambayo unaweza kuyapata kutokana na kula chakula kibovu au kilichoharibika, wakati mwingine waweza hata kupoteza maisha. Turudi katika uhalisia sasa, hapa kwa wale ndugu zangu wakulima nadhani mtanielewa zaidi, hivi toka lini mtu akaipanda mbegu mbovu na akategemea mavuno mengi ya kuzii?. Unajua ni kwanini wakulima huchambua mbegu zao kabla ya kuzipanda au unajua ni kwanini wakulima huitaji mbegu bora? Jibu ni rahisi wakulima uchambua mbegu nzuri ili wasipande mbegu ,bovu kwa kuwa wanajua kuwa mbegu mbovu kamwe haiwezi kuzaa matunda na kama ikizaa matunda hayo yatakuwa mabaya.

Sasa chukua mfano huu wa mbegu mbovu ubadilishe jina lake na mifano yake, yaani badala ya mbegu mbovu weka fikira mbovu (hasi). Kwanini ulalamike usiku kucha, mchana kutwa kuwa maisha magumu, maisha hayaendi kila unachofanya hakieleweki na unakalia kumlaumu mungu kuwa kawapendelea wengine nk. Kumbe tatizo ni fikira zako mbovu ndizo zinakuletea matatizo yote hayo. Kama ilivyo katika mbegu kuwa mbegu mbovu haizai basi hata katika fikira ni hivyo hivyo nini cha kufanya sasa cha kufanya ni kufutilia mbali fikira mbovu.
Mbegu bora /fikira njema(chanya), mbegu bora ni ile yenye kuzaa matunda mengi tena kwa wingi sana, hii ni mbegu ambayo haina  takataka za aina yoyote yaani ni mbegu ambayo ni safi sana na hivyo mpandaji huipanda pasipo kuwa na wasiwasi wowote ule juu ya uotaji na kipato. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa fikira njema au chanya, mtu mwenye fikira chanya hana wasiwasi na maisha yake maana anaamini kuwa karanga iliyopandwa huzaa karanga inayofanana na mbegu husika na wala karanga haiwezi kuzaa mchungwa. Fikira njema haina takataka kama vile woga, ukataji tama, uhairishaji wa mipango ovyo vyo, majungu wala upotezaji wa muda ovyo.
Ni vyema ukajijengea fikira njema au chanya ili usiishi kwa wasiwasi, chagua mbegu bora ili uwe na uhuru na masiha yako. Ikiwa unaishi tu pasipo kuchagua aina ya mbegu inayokufaa basi aina yoyote ile ya matokeo kubaliana nayo lakini nakutaadharisha na uzingatie kuwa hauwezi kuvuna ambacho hukupanda hivyo chunguza matokeo ya mambo yako kisha utajua aina gani ya mbegu umepanda. Nakutakia kila kheri katika safari yako ya kuyaelekea mafanikio.
Ni mimi Rafiki yako,
Baraka maganga.
Bmaganga22@gmail.com
0754612413/0652612410.


Tuesday, November 24, 2015

Ni Wewe Wa Kufanya Hakuna Mwingine.


Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu, ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri katika jitihada za kuhakikisha unapambana vikali ili tu kujiletea mafanikio na maendeleo nami nakusihi endelea kuwasha moto huo ulio ukoka ili tu usizime.
Kama kawaida tumekutana hapa lengo ni kutaka kupeana maarifa mapya na leo somo letu/ mada yetu inasema ni wewe wa kufanya na sio mwingine.
Kabla sijaenda mbali nataka ujiulize hili swali je? Unahisi kuna mtu alikuja duniani ili akufanyie jambo Fulani, akupangie mipango, malengo na akuangaikie kila siku ili kutatua matatizo yako. Kama jibu ni hapana, sasa unazani nani yupo ili kufanya kazi zako, kupanga mipango yako, malengo yako n.k. natumaini jibu ni kuwa hakuna mwingine wa kufanya vitu hivyo Bali ni wewe hakuna mwingine bali wewe unaesoma makala hii.
Tambua kuwa kila binadamu anamipango yake, malengo yake, shughuli zake, mawazo yake na fikira zake juu ya maisha yake. Tumekuwa tukiambiana kuwa daaa! Rafiki,ndugu au mwanangu nilikuwa nikikufukiria sana muda mrefu. Hivi unadhani anayekuambia kuwa nilikuwa nakufikiria au anakuwaza aliacha shughuli zako na kuanza kukuwaza tu wewe? Unafikiri wewe unaumuhimu mkubwa sana kwa huyo mtu mpaka aanze kukuwaza wewe sasa kama unategemea au unaamini kuwa kuna mtu anakufikiria umepotea sana tambua hakuna mtu wa kuwazia shughuli zako, wala mikakati yako mingine bali ni wewe mwenyewe yaani usijidanganye kuwa kuna mtu atafikiria juu ya maisha yako hakuna hicho kitu. Atafikiri sawa lakini hawezi kufikiri ama kuwaza kama ambavyo wewe ungefikiri na kuwaza juu ya maisha yako.
Unakaa hutaki kujishughulisha kabisa hutaki kufanya kazi yoyote unategemea watu fulani wakufanyie shughuli hizo hivi unafikiri kuna mtu ni mtumwa wako ambae atakuwa akikufanyia tu shughuli zako huku wewe umekaa tu ukisubiri akufanyie. Unafikiri bado kuna mfumo wa maisha unaoitwa utumwa? Nakuambia hakuna mfumo huo ulikwisha zamani sana pamoja na biashara ya utumwa hivyo leo hii hauwezi kumfanya mtu mtumwa wako kiurahisi. Hivyo tambua kuwa hakuna wa kukufanyia shughuli zako hivyo basi. Inuka ukajishughulishe acha kuona kuwa kuna mtu atakufanyia kazi. Hakuna mwingine wa kukufanyia shughuli bali wewe wenyewe.
Unafikiri kuna mtu maalumu ambaye yupo kwa ajili ya kukupangia malengo yako. Kama unaamini mtu huyo yupo na umempata basi tambua kuwa umepotea na unajidanganya maana hakuna mwingine wa kupanga malengo yako, bali ni we we. Tambua hilo kuanzia leo na ulishike. Malengo bora ni yale ambayo umeyapanga mwenyewe maana utakuwa pindi unapoyasoma yanakuhamasisha na kukumbusha kuwa ni wewe mwenyewe uliye ya panga na kuyaandika hakuna mwingine. Hivyo basi usimruhusu mtu akupangie malengo maana ukifanya hivyo yule anayekupangia malengo ataandika malengo yake na atakuaminisha kuwa hayo malengo ni yako. Hivyo wewe utayafata hayo ukiamini ni yako kumbe umepotea sana tena sana. Hivyo basi tambua kuwa malengo bora ni yale uliyojipangia mwenyewe.
Usipende kujidanganya kuwa fulani ananijali sana huwa anafanya hili na lile kwa ajili yangu, hivyo basi sina haja ya kufanya jambo hilo kwa kuwa kuna mtu yupo anafanya hilo kwa ajili yangu. Nikuulize kitu hivi unauhakika kuwa  huyo anayekufanyia hayo mambo mnaendana kiakili, fikira,mtazamo, ubunifu?n.k. kama jibu ni hapana sasa kwanini unamwachia akufanyie. Acha Mara moja na fanya mwenyewe maana mnatofautiana kiufanisi, ubunifu, akili, uwajibikaji nk.
Ni muhimu utambue kuwa hata ukubwe ma matatizo kiasi gani mwenye nafasi ya kutatua matatizo yako ni wewe na sio mwingine. Una nafasi kubwa sana ya kujihusisha na matatizo na changamoto zinazokukabili tofauti na mtu mwingine yoyote. Hivyo basi wa kuwajibika na changamoto zako ni wewe sio mwingine. Daktari pekee hatoshi kukuponya ila uwepo wa daktari na imani yako ndio vitu vya kukuponya wewe hata kwa yale magonjwa yanayoonekana hayawezekani kutibika.
Tambua kuwa haukuja duniani ili ufanyiwe kitu Fulani. Bali ulikuja duniani ili ufanye jambo au mambo Fulani. Hivyo basi kuanzia leo tambua kuwa hakuna mwingine wa kukufanyia bali ni wewe mwenyewe.
Ni Mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.
0754612413/0652612410.


Monday, November 23, 2015

Kitu Hiki Kimoja Kinatushinda Wengi Na Kuturudisha Nyuma.


Habari za Siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa, mtandao ambao umejidhatiti katika kuhakikisha unakupa maarifa mapya kila Siku na kukusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha yako na kuifanya safari yako ya kuelekea mafanikio isiwe ya kukuchosha na kukatisha taama. Ambatana nami katika makala ya leo ili ujue leo nimekuletea kitu gani kipya.



Mara nyingi sana binadamu tumekuwa ni watu wa kupanga mambo mengi sana juu ya maisha yetu, tumekuwa ni mabwana mipango, na wengi tumekuwa wenye kuweka mipango mingi sana lakini shida inakuja pale ambapo inatupasa tutekeleze hiyo mipango yetu. Asilimia kubwa sana ya watu tumekuwa wenye kuweka mipango mingi na malengo mengi yasiyotekelezeka yaani wengi wetu mipango yetu na malengo yetu hubaki vichwani mwetu au katika karatasi za daftari ambamo huwa tunakuwa tumeandika na kuhifadhi mipango na malengo yetu hayo. Tumekuwa ni kina bwana panga pangua hii ni kutokana na sababu kuwa tumekuwa tukiweka mipango hii na malengo yale lakini ghafla tunaivunja na kuweka mipango mingine mipya. Huu umekuwa mchezo wa tulio wengi sana. Je? Unajua nini kinatufanya tuwe hivyo. Kama haujui basi ambtana nami. Kuna sababu moja kuu ambayo imekuwa ikifanya hali hii itokee nayo ni kushindwa  kujitoa kisawasawa.
Utekelezaji wa mipango na malengo yetu vinahitaji kujitoa kisawasawa, kupanga malengo yetu na mipango yetu kisha kuiandika katika vijitabu vyetu vya kumbukumbu zetu haitoshi kutufanya au kutuonesha wenye mafanikio. Ili utekeleze mipango yako na malengo yako ni lazima ujitoe kweli. Kuandika malengo au kupanga mipango yako hakukufanyi uwe mwenye mafanikio bali utekelezaji wa mipango na malengo husika ndio hutuletea mafanikio.
Baada ya kuwa umepanga malengo na mipango yako na ukaamua kuitekeleza kisawasawa, ukaanza kuifanyia kazi mipango hiyo lakini kila unapojaribu kuitekeleza mipango hiyo unajikuta umeshindwa kuitekeleza, unajaribu tena kwa Mara ya pili unashindwa, unajaribu tena na tena lakini matokeo yanabaki vile vile. Unajua kwanini hali hii inajitokeza?
Hali hii inajitokeza kwa kuwa ndio umepanga mipango na malengo yako vizuri lakini hujajitoa kikamilifu katika kuhakikisha unayatimiza Yale uliyoyapanga, ndio hujajitoa kisawasa pengine unasema hapana Mimi mbona najituma katika shughuli zangu nafanya hivi na vile ili kutekeleza yale niliyojiwekea na kujipangia lakini sipati matokeo mazuri kwanini inakuwa hivi. Jibu ni kuwa hujajitoa kisawasawa.
Unaweza kujiona umejitoa kisawasawa katika kutekeleza mipango na malengo yako lakini kumbe ndani ya kule kujitoa kwako kumeambatana na hali ya uvivu hivyo ule uvivu unakufanya usifanye kazi kwa kiwango kile kinachotakiwa ili kukuwezesha kuyatekeleza Yale malengo yako. Ikiwa unafanya shughuli zako na unajiona kuwa unaweka jitihada za kutosha kuyatekeleza Yale uliyojipangia lakini matokeo yanakuja tofauti na ulivyotegema jua kuwa hujajitoa kisawasawa, kunasehemu ambayo unafanya shughuli kivivu na ndio maana unashindwa kupata matokeo mazuri.
Endapo utapanga mipango yako vizuri na ukajitoa kisawasawa basi nakuhakikishia kuwa utafanikiwa kwa kiasi kikubwa hakuna jambo ambalo litakufanya usipate matokeo Yale ambayo uliyategemea, maana kujitoa kutakusaidia wewe kuondokana na hali ya uvivu, kukata tamaa na visingizio vya hapa na pale.
Unapoweka mipango na malengo yako hakikisha umejitoa kisawasawa katika kuyatekeleza usiweke tu mipango kisha ukaacha tu mipango inaelea elea, na utambue kuwa mipango haiwezi kujitekeleza yenyewe.
Ni Mimi rafiki yako.
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.

0754612413/0652612410.

Sunday, November 22, 2015

Ni Wao Sio Wewe, Ni Wewe Sio Wao

.
Kama wameshindwa ni wao sio wewe. Kushindwa kwa watu kusikufanye nawe ushindwe. Binadamu tumeubwa sawa haya ni maneno ya watu wengi lakini unaposema binadamu tumeubwa sawa ni neno pana kidogo maana huo usawa unaouzungumzia wewe ni katika mawanda yapi. Mfano leo hii ukisema binadamu ni sawa kiakili huoni kama unakosea, maana binadamu tunatofautiana sana tena sana ndio maana kuna warefu, wafupi, weupe, weusi, wenye ulemavu na wasio n.k. wale ambao wanaamini kuwa binadamu ni sawa ndio hutumia watu wengine kama marejeleo yao kwa kiasi kikubwa tena sana ndio maana wao huamini kuwa kama mtu fulani alishindwa basi nao watashindwa kwa kuwa binadamu wote ni sawa. Mara nyingi watu hawa huwa ni wenye mtazamo hasi kwa kuwa wao huamini kuwa binadamu ni sawa na inapotokea mtu fulani anataka kufanya jambo Fulani sawa na mtu au watu Fulani kwa kuwa wao wanamtazamo hasi basi hukimbilia haraka kwenye marejeleo ya watu walioshindwa na sio waliofanikiwa. Hii ni kutokana na mtazamo wao hasi.
Nimekueleza kuwa kauli ya kusema kwamba  binadamu wote ni sawa ni kauli pana sana( it is a general term) maana inabidi ueleze huo usawa wako upo katika mawanda yapi? Nafikiri tuseme binadamu ni sawa kwa namna ya uumbaji wao na ukuaji mfano tunaweza kusema binadamu aliubwa na mwenyezi mungu kama vile washikadini wa dini zote tunavyoamini, pia binadamu wote ni sawa kwa kuwa wote huzaliwa na mwanamke hapo pana usawa, binadamu ni sawa katika makuzi yao maana wote huzaliwa na wakiwa hawana uwezo wa kuongea, huanza kutambaa, kutembea hatimaye kuongea. Huwa watoto, wakawa vijana, wakazeeka na hatimaye wakafa. Hivyo ni sawa kwa binadamu wote maana hakuna binadamu ambaye aliwahi kuwa mzee kisha akarudi ujana kisha utoto hapajawahi kutokea kitu kama hicho hapa duniani. Sasa unaposema binadamu wote ni sawa lazima utueleze usawa huo upo katika mawanda yapi?
Binadamu ni sawa katika mawanda ambayo nimekuonyesha hapo juu, lakini nini kimeniasukuma sasa mpaka nikuambie ni wao sio wewe na ni wewe sio wao, hapa namaanisha kuwa kama wameshindwa au walishindwa niwao na sio wewe na kama umeshindwa ni wewe sio wao. Nachotaka kusema hapa ndugu msomaji ni kuwa tambua kuwa binadamu tunatofautiana katika mawanda mbalimbali kama ilivyo katika kufanana, mawanda hayo ndio huleta utofauti miongoni mwetu na ndio maana nimesema ni wao sio wewe na ni wewe sio wao. Nakuletea mawanda hayo ili unielewe zaidi,
1. Utendaji, tunaweza kuwa tunafanya kazi sawa lakini utendaji wetu wa kazi ukawa tofauti kabisa ndio maana waalimu wawili mfano wanaofundisha somo moja wanaweza kutofautiana ambapo itatokea mmoja akaeleweka zaidi kuliko mwingine. Hii ni kutokana na utendaji wao kutofautiana hivyo kutokana na mawanda ya utendaji tunaweza kusema ni wao sio wewe na ni wewe sio wao. Yaani kama wameshindwa/wameweza ni wao, na kama umeshindwa/umeweza au kufanikiwa ni wewe sio wao.
2. Uwajibikaji, binadamu tunatofautia kiuwajibikaji hivyo uwajibikaji wa mtu mmoja na mwingine ni tofauti sana kutokana na utofauti huu wa kiuwajibikaji utakutana na makundi matatu ya watu ambapo la kwanza ni wanawowajibika sana, pili wanawowajibika wastani na tatu na mwisho ni wale wenye uwajibikaji mbovu. Hivyo ndivyo tunavyotofautiana kiuwajibikaji.
3. Fikira, binadamu tunatofautiana kifikira sana tena sana, kuna wengine wana fikira potovu na wengie hawana fikira potofu hivyo kama wanafikira potovu/sahihi ni wao sio wewe na kama unafikira potovu/sahihi ni wewe sio wao.
4. Mtazamo,binadamu tunatofautiana kimtazamo tena kwa kiasi kikubwa sana. Kuna wale wenye mtazamo hasi na wale wenye mtazamo chanya tofauti hizi za kimtazamo huamua tofauti za matendo yetu. Yaani mtu mwenye mtazamo hasi huwa na matendo yenye kuendana na mtazamo wake na yule mwenye mtazamo chanya pia huwa na mtazamo wenye kuendana na mtazamo wake. Hivyo kama wanamtazamo hasi/chanya ni wao sio wewe na kama unamtazamo hasi/chanya ni wewe sio wao.
5. Kiwango cha uvumilivu, hapa pia tunatofautiana sana. Tunaweza kuugawa uvumilivu wa binadamu katika makundi makuu matatu ambapo tutapata uvumilivu mkubwa, wastani na mdogo. Kila aina ya uvumilivu una watu wake hivyo basi kama upo kwenye aina Fulani ni wewe na sio wao na kama yupo kwenye aina Fulani ya uvumilivu ni yeye sio wewe.
6. Umakini, binadamu tunatofautiana katika kiwango cha umakini ambapo wengine ni makini sana na wengine sio makini sana. Ndio maana utawasikia watu wakisema yule jamaa ni mtu makini katika utendaji kazi wake wakati utasikia mwingine akisema yule jamaa hayupo makini kabisa katika utendaji kazi wake.
Sikuandika makala hii ili kukutofautishia tabia za binadamu bali nimeandika makala hii ili kukufungua na kubwa zaidi kukusihi uache kutumia watu kama marejeleo tena watu walioshindwa badala yake jijengee mazoea ya kujiamini na amini kuwa binadamu tunatofautiana sana hivyo basi kama umeshindwa ni wewe na kama wameshindwa ni wao. Pia wewe ulieshindwa usitake kujitumia kama mfano na uwafanye watu waamini kuwa watashindwa kama wewe. Kumbuka ni wao sio wewe na ni wewe sio wao. Zaidi usiruhusu historia ya mtu ikukatishe tamaa maana sio yako ni yake.
Ni Mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.
0754612413/0652612410.


Tuesday, November 17, 2015

Je Waijua Picha Unayojijengea Akilini Mwako?


Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa mtandao ambao upo ili kuhakikisha kuwa unapata mambo mazuri ya kukujenga na kukuhamasisha. Leo nataka kukushirikisha jambo lifuatalo:-
Kwa kawaida binadamu amekuwa ni mtu wa kufikiria mambo mengi juu ya maisha yake. Kutokana na fikira hizo hapo ndipo binadamu huwa anajijengea picha mbalimbali juu ya maisha yake. Picha hizi huendana na fikira za mwanadamu kwa kiasi kikubwa sana. Yaani kama mtu anawaza fikira hasi na kuyaona maisha kwa mtazamo hasi basi picha zote atakazojijengea akilini mwake zitakuwa ni picha hasi ambazo zimejaa kushindwa, visingizio, woga na vipingamizi kadha wa kadha. Wakati kama mtu anawaza fikira chanya atakuwa na mtazamo chanya na hivyo atajijengea picha za ushindi, na mafanikio kwa kila anachokifanya n.k.
Je picha hasi zinatoka wapi?
Picha hasi hutokana na fikira hasi ambazo chanzo chake kikubwa chaweza kuwa kauli za wazazi wetu, ndugu wa jirani au marafiki wa karibu nasi. Mara nyingi watu wanaotuzunguka huwa wana madhara makubwa sana kwetu, madhara haya yaweza kuwa hasi kama nao ni hasi au chanya kama wao wanakauli chanya. Mara nyingi tumekuwa ni watu wa kuamini sana kwa yale ambayo tumekuwa tukiambiwa na watu wa karibu nasi jambo ambalo muda mwingine huweza kutuletea madhara makubwa sana. Katika hali ya kawaida mtoto ambaye amekuwa katika hali ya kusemwa kuwa huna akili, wewe ni mbumbumbu, huwezi lolote pindi anapokuwa amekuwa mtu mzima huwa anachukulia kauli hizi kama ukweli wa maisha yake halisi na hivyo kujijengea picha hasi kichwani mwake ambazo humfanya ajione hawezi lolote na nimbumbumbu haswa.
  Ndugu msomaji ni muhimu uelewe vizuri aina ya picha ambazo unajijengea. Kwa kuwa wote tunahitaji mafanikio makubwa maishani basi tusiende kinyume na kanuni za mafanikio kama kanuni hii rahisi ambayo inaseama huwezi kujijengea picha hasi na ukapata matokeo chanya au picha chanya na ukapata matokeo hasi. Yaani ni sawa na mkulima alimaye mtama hutegemea kuvuna mtama na sio ulezi. Kama akipanda mtama akitegemea kupata ulezi basi mkulima huyu atakuwa na matatizo makubwa.
  Kimsingi kama unataka kuendelea na kupata mafanikio makubwa jijengee picha chanya ili zikuletee matokeo chanya lakini kumbuka picha chanya inatokana na fikira chanya. Na picha chanya ni ile hali ya kujitabilia au kujionea maisha yako katika hali yakushinda wakati picha hasi ni ile Hali ya kujionea maisha katika kushindwa.
Ni mimi rafiki yako.
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.
0754612413/0652612410.


Unajiua Kila Siku Kwa Kufanya Jambo Hili Mara Kwa Mara.




Habari za siku ndugu msomaji WA mtandao huu wa kona ya maarifa, ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri katika harakati zako za kujiletea mafanikio.
Leo nakushirikisha jambo hili ambalo wengi wetu tumekuwa tunalifanya ambapo Nina uhakika wengi wetu hatujui madhara yake ndio maana tumekuwa tukilifanya. Jambo lenyewe ni kutaka kumridhisha kila mtu.
Tabia ya kutaka kumridhisha kila mtu imeshamili sana miongoni mwetu ambapo watu wengi tumekuwa tukifanya mambo mbalimbali ambayo wakati mwingine tunakuwa hatuyataraji, wala kuyapenda lakini tunayafanya,  hii ni kwasababu tu tunataka kuwaridhisha watu. Tumejijengea fikira za kutaka kuwaridhisha wazazi, wadogo zetu, majirani na ndugu mbalimbali. Wakati tukifanya hivi tumejikuta tukisahau hata kufanya mambo yetu ya msingi kisa tu tunataka kuwaridhisha watu.
  Sio jambo la ajabu kumkuta mtu anaacha shughuli yake ya msingi na kwenda kumsaidia mwingine shughuli kisa tu aonekane mwema na mwenye fadhira kwa mtu huyu, huku akilini mwake akiamini kuwa amemuridhisha yule mtu kwa msaada wake, lakini wakati huo huo amesahau kuwa alikuwa na shughuli yake ya msingi ambayo aliiacha kisa tu amsaidie huyu mtu. Lakini nataka ujiuluze kama umeona kuacha shughuli zako na kuwasaidia wengine ndio njia ya kuwaridhisha hao watu, piga hesabu hapo unapoishi kuna watu wangapi?, na kwa kuwa unataka kumridhisha kila mtu na njia uliyochagua kuwaridhisha watu hawa ni kwa wewe kujihusisha na shughuli zao huku ukiacha shughuli zako piga hesabu kama unapoishi kuna watu mia tana (500), utakuwa na siku ngapi za kuwasaidia na nilini haswa utajihusisha na shughuli zako?.
Ki kawaida binadamu ni kiumbe aliye mgumu kuridhika yaani ni ngumu sana kumridhisha binadamu kwa kuwa binadamu amejaa lawama na kama binadamu wengi wa sasa wamejaa lawama basi hutoweza kuwaridhisha wote. Maana hata kwa ile njia ambayo umeichagua kuwa utawaridhisha kwa kuwasaidia shughuli zao wapo ambao hawataridhika maana wanaweza kutumia kigezo cha muda na uzito wa shughuli ambapo watakuhukumu kuwa kunabaadhi ya watu ulitumia muda mwingi kuwasaidia tofauti na wengine hivyo basi hawajaridhika sasa jiulize utafanyaje kuwaridhisha watu hao?. Pengine utataka kurudia kwa wale unaona hawajaridhika utakapo rudia utakuwa ndio umejiloga maana ukirudia kuwasaidia na wengine tena watasema nao pia hawakuridhika. Hapo ndipo utakapo gundua kuwa binadamu ni kiumbe asiye ridhika kiurahisi.
Jiulize mwenyewe ni Mara ngapi wewe uliyeajiriwa umekuwa ukiamua kufanya maamuzi magumu ya kugawana mshahara wako na wazazi,marafiki au wadogo zako. Hivyo basi kila unapopata mshahara unawagawia kiasi cha pesa huku ukiamini kuwa kwa kufanya hivyo umewaridhisha na kuwafurahisha lakini nakuambia ukweli kwa binadamu wa sasa ambao ni wajaa lawama watakulaumu tu, na watadiriki hata kusema kuwa hauwasaidii. Ili hali wewe unawasaidia. Hivyo basi kama unatoa msaada toa kwa sababu umeamua kusaidia na sio kwa lengo la kuwaridhisha watu.

Tambua jambo moja haukuja duniani kumridhisha mtu wala kupendwa na kila mtu hivyo basi jambo la msingi kwako ni kuwa tenda haki siku zote usiwe mtu wa kuyumba yumba bali tenda haki siku zote. Pia weka malengo yako na hakikisha unayatekeleza kwa namna yoyote ile.
Ni Mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.
0754612413/0652612410.



Posted via Blogaway


Thursday, November 12, 2015

Hiki Sio Kipimo Halisi Cha Mafanikio Yako.


Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu. Ni matumaini yangu unaendelea vizuri katika harakati zako za kupambana katika kuyatimiza yale uliyokwisha kujiwekea kama malengo yako. Tumekutana tena katika kutaka kuelimishana na kujengana yote haya ni katika kuhakikisha kuwa safari yetu ya kuyaelekea mafanikio inakuwa bora zaidi na zaidi.

 Leo ndugu msomajia nataka kukushirikisha jambo moja ambalo binafsi naliona ni kama imani potofu ambayo inaendelea kupandikizwa miongoni mwetu. Imani hii in ile yenye kutufanya tuamini kuwa mafanikio yako mjini tu na hivyo basi kijijini hakuna mafanikio.

 Tumekuwa ni watu wenye kuamini kuwa watu wanaoishi mjini ndio wenye mafanikio tofauti na wale wanaoishi vijijini, sidhani kama jambo hili lina ukweli wowote japo kuwa kiukweli ni kwamba ukilinganisha mafanikio ya mjini na mafanikio ya kijijini ni dhahiri mjini.

 kunaonekana kuna mafanikio lakini hapa tunazungumzia mafanikio ya mtu mmoja mmoja. Ukiangalia leo hii utagundua kuna Lindi kubwa sana la watu (haswa vijana).ambao wanahama kijijini kuelekea mjini wakiamini kuwa mjini ndiko kwenye mafanikio tofauti na kijijini. Lakini wengi wao wakifika mjini hukuta mambo yamekuwa magumu sana kiasi kwamba hutamani kurudi tena kijijini.

 Kimsingi mafanikio yana husisha fursa jambo la msingi ni kutafuta fursa na kutumia fursa hizo, leo hii utamkuta mtu akikimbia kijijini huku akitelekeza mashamba mengi sana na kuamua kwenda mjini kutafuta kazi, mtu huyu ameamua kwenda mjini kwa kuwa ameaminishwa kuwa mjini ndiko kwenye mafanikio lakini mafanikio sio wingi wa watu, magorofa, magari n.k. mafanikio ni pale ambapo umeweza kuyatekeleza malengo yako binafsi na uwezo wa kutekeleza malengo hauna uhusiano na niwapi haswa ulipo. Yaaani hakuna sheria ya kwamba ukitekeleza mafanikio yako ili hali uko mjini ndipo watakuita mwenye mafanikio na kama ukitekeleza malengo yako ili hali ukiwa kijijini hautaitwa mwenye mafanikio.

 Jifunze kuchunguza fursa mahali ulipo na uzitumie usiwe mtu wa kukurupuka na kukimbilia sehemu zingine huku ukiamini sehemu hizo ndizo zenye mafanikio kuliko zingine pasipo kufanya tathimini yoyote ya msingi.

Ni Mimi rafiki yako
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.
0754612413/0652612410.


Wednesday, November 11, 2015

Jifunze Jinsi Ya Kuyatumia Mafanikio Ya Wenzako.


Habari ndugu msomaji wa mtandao huu. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri na harakati za hapa na pale huku ukiwa na hamasa kubwa sana ya kuyapata mafanikio nami nasema vizuri na endelea kupambana.
 Leo nataka nikushirikishe jambo nalo ni kuhusu jinsi ya kuyatumia mafanikio ya wengine. Kuna namna mbili ambazo binafsi nimeziona watu wakiyatumia mafanikio ya watu.

1. Mafanikio ya watu kama chanzo cha mgogoro, kuna watu wanatumia mafanikio ya watu kama chanzo cha mgogoro baina yao na ya watu wenye mafanikio. Yaani hapa namaanisha kuwa kuna watu ambao hawapendi mafanikio ya watu hawa ni watu ambao hawapendi kuona watu/ mtu Fulani kafanikiwa hivyo basi watu hawa huanza kuwashutumu watu wenye mafanikio kwa maneno na vitibwi kemukemu. Watu hawa huwa ni wenye kutawaliwa na wivu na roho mbaya sana, hivyo huona kufanikiwa kwa wengine sio haki. watu hawa huwa ni wenye mtazamo hasi mara zote juu ya mafanikio ya wenzao na pengine huona ni kama watu wenye mafanikio husika hawasitahiri kuyapata mafanikio hayo.

2. Mafanikio ya watu kama somo, aina ya pili ya watu ni wale ambao huchukulia mafanikio ya wenzao kama somo, hawa ni wenye kufurahia mafanikio ya wenzao na kuwaona watu waliofanikiwa kama watu wenye kuwa darasa kwao, msaada na kimbilio kwao. Aina hii ya watu ni wale ambao hudiriki kuwafata watu wenye mafanikio na kutaka kujifunza kwao kuwa wamefanyafanya vipi au wamepitapita vipi mpaka kuyafikia mafanikio. Hawa ni ambao hutaka kujifunza zaidi kupitia waliofanikiwa na hutaka kuwa kama waliofanikiwa.

 Nimekupatia njia mbili za kujifunza kupitia watu walifanikiwa lakini nakushauri utumie njia ya pili kwa kuwa ndio bora na yenye msaada kwako kama kweli unataka kufanikiwa.

 Ni Mimi rafiki yako
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.

0754612413/0652612410

Tuesday, November 10, 2015

Zijue Njia Sita (6) Za Kujifunza.


Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa. Kama ilivyokawaida kila tunapokutana hapa huwa tunakutana kwa lengo la kupeana maarifa mapya ambayo yatatusaidia na baadae kutuletea mafanikio.

 Baadhi tumekuwa tukiamini kuwa njia bora ya kujifunza ni ya  sisi kwenda shuleni kisha mwalimu anakuja anasimama mbele yetu na kuanza kutufundisha mambo mbalimbali. Wengi tunaamini kujifunza kupo shuleni tu. Kujifunza kwa njia ya shule ni njia ya hasili na njia hii hutufanya wakati mwingine tukose uelewa wa mambo ya msingi kuhusu maisha. Chukulia mfano wewe unaetegemea elimu ya kutoka shuleni utajifunzaje elimu kuhusu pesa maana shuleni hakuna somo la pesa. Sasa kama jibu ni huwezi kujifunza elimu ya pesa kutoka shuleni basi zijue njia nyingine zifuatazo ambazo zitakusaidi kujifunza mambo mengi sana tofauti na yale ya shuleni.

1. Kutazama, hii ni njia mojawapo ya kujifunza mambo mengi sana na jambo la kushangaza ni kwamba njia hii ni rahisi na haina gharama kubwa sana lakini ndio njia ambayo haitumiki na wengi.Njia hii ni nzuri sana maana inahusisha kutazama shughuli aifanyayo mtu Fulani kisha ukajifunza jambo. Mfano unaweza kumtazama fundi selemala jinsi anavyounganisha mbao mpaka kupata mlango hivyo ukawa umejifunza jambo Fulani na taratibu ukilifanyia kazi utajikuta nawe unauwezo wa kuunganisha mbao na kupata mlango kama alivyokuwa akifanya selemala uliyekuwa unamtazama. Hivyo basi jifunze kupitia njia ya kutazama.

2. Kusoma vitabu, vitabu vinasiri nyingi sana kuliko wengi wetu tunavyofikiri. Vitabu hivi daima huwa vinaandikwa na wataalamu na watu waliofanikiwa kimaisha ambapo huandika kwa lengo ya kufunza kuhamasisha, na kutia motisha maishani. Lakini kitabu cha kwanza katika kuhamasisha ni biblia kwa wakristo na kwa waislamu ni kuruani. Vitabu vimejaa mambo mengi ambayo huwezi kuyapata shuleni kama unavyotegemea, vitabu vimejaaa historia za watu waliofanikiwa, changamoto zao, maisha yao mpaka kufanikiwa na baada ya kufanikiwa. Pia kuna vitabu ambavyo vimejaaa elimu kuhusu pesa mfano wa kitabu hicho ni kitabu cha rich dad poor dad cha bwana Robert kiyosaki. Hivyo basi jenga utamaduni wa kujisomea angalau kitabu kimoja kwa wiki.

3. Video, Leo hii unaweza kujifunza mambo mbalimbali kupitia video za wataalamu mbalimbali. Leo hii kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia wataalamu wamekuwa wakifundisha mambo mbalimbali ambayo hurekodiwa na kuwekwa katika mitando kama vile YouTube ambapo unaweza kuzitazama video hizo na kujifunza. kama unahisi unaelewa zaidi kwa njia ya video kuliko zingine basi tumia njia hii ya video katika kujifunza kwako. Leo hii kuna baadhi ya mambo mfano kuhusu komputa unaweza kujifunza kwa kupitia kuangalia video fupi za YouTube.

4. Semina, hii ni njia nyingine ambayo kwa hapa kwetu Tanzania imeibuka hivi karibuni. Njia hii imeshika kasi sana na kuonekana ni bora sana na ni rahisi kwa kiasi Fulani. Semina zimegawanyika ambapo zipo semina za bure na za kulipia. Usiogope kutoa pesa na kwenda kwenye semina mbalimbali, Bali nakushauri tumia pesa yako katika semina na hautokuja jutia hilo. Nakuambia hivyo kwa kuwa Nina uhakika semina zinafundisha mambo mengi mazuri ambayo usingeweza kuyapata shuleni na kwingineko.

5. Kanda za kunasia sauti/ tepu rekoda, hii ni njia nyingine sawa na njia ya video ila tofauti ni kuwa video huhusisha sauti na picha ila njia hii haihusishi sauti na picha. Hivyo basi kama unahisi hauwezi kujifunza kwa kupitia njia ya video au kusoma vitabu maana kuna vitabu ambavyo huwekwa katika mfumo wa sauti(audibook) ambapo unaweza kuyapata Yale yaliyomo kwenye kitabu kwa njia ya kusikiliza.

6. Kuwauliza wataalamu. Kila unachotaka kujifunza kuna watu wanakijua na watu hawa ndio hufahamika kama wataalamu. Wataalamu hawa hawapo kwa ajili ya kujisifia au kusifiwa juu ya utaalamu wao Bali wapo ili kuwasaidia watu ambao wanashida na vitu ambavyo wao ndio wanautaalamu navyo. Unapotaka kujifunza jambo na ukahisi unahitaji ushauri wa kitaalamu basi fanya hivyo ili uweze kujifunza kupitia wataalamu hao.

 Nimekuorodhoshea njia hizo sita za kujifunza tofauti na shuleni. Simaanishi kuwa watu wasiende shuleni kujifunza Bali maana yangu ni kuwa watu wasitegemee shule pekee maana shule pekee haitoshi, hivyo watumie na njia hizi katika kujifunza Yale ambayo Nina uhakika shuleni hayapo mfano elimu juu ya pesa.

Ni Mimi rafiki yako
Baraka maganga.
Bmaganga22@ gmail.com.

0754612413/0652612410.

Tegemea Kukutana Na Watu (5) Wa Namna Hii Katika Safari Yako Ya Mafanikio

.
Habari za wakati huu ndugu mpenzi msomaji wa mtandao huu. Ni matumaini yangu kuwa hu mzima na mwenye nguvu nyingi za kupambana ,hii yote ni katika kuhakikisha unajiletea mafanikio. Nami nakusihi endelea kupambana pasipo kuchoka. Leo nataka kukuletea aina zifuatazo za watu ambao utegemee kukutana nao. Katika safari yako ya kuelekea mafanikio


1. Wakatisha tamaa, tegemea kukutana na watu ambao watakukatisha tamaa sana kwenye safari yako ya mafanikio, watakuambia huwezi kwa kuwa elimu yako ndogo, watatumia umri wako, watatumia kabila lako, mkoa unaotoka n.k. watu hawa wapo tu na kama wakikushinda watakufanya usiende mbele na matokeo yake ukate tamaa na kushindwa. Hivyo basi pindi wanapokuja watu hawa hakikisha hawakushindi na kuwa sababu ya wewe kutokufanikiwa.

2. Watakao kucheka, kuna muda utakapoanzisha jambo Fulani kuna watu watakucheka sana na kukuona mjinga au mwendawazimu lakini jambo hili lisikufanye ukarudi nyuma katika safari yako ya kuelekea mafanikio. Lakini jambo moja ambalo nataka kukushauri ili uepukane na hali ya kuchekwa ni kuwa usipende kumwambia kila mtu malengo yako Bali mwambie mtu unaemwamini ili akushauri na sio kukuvunja moyo.

3. Watakao kupinga, wapo watu watakaokupinga sana na kukuwekea vizuizi mbalimbali katika safari yako ya mafanikio. Watu hawa sio kuwa hawajui kuwa unaweza kufanikiwa Bali wanajua kuwa unauwezo wa kufanikiwa tena sana, muda mwingine wanakuwa wanajua kuwa unaweza kufanikiwa mpaka ukawazidi wao na ndio maana wanakupinga kwa kuwa wanakuogopa. Mara nyingi anae kupinga anakuwa na sababu kuu mbili za kufanya hivyo aidha anaogopa utamzidi baada ya wewe kufanikiwa au ana wivu.

4. Watakao kuunga mkono, sio wote watakaokupinga wapo watu watakao kuunga mkono tena sana. Mara nyingi watu hawa ni watu wetu wa karibu kama vile wazazi, walezi, marafiki na wakati mwingine huwa watu ambao huwa tunakuwa hatuwajui ila tunakutana nao tu katika shughuli zetu na wanaungana na sisi ili tu kuhakikisha tunakuwa pamoja katika kujiletea mafanikio.

5. Watakao kushauri, utapokea ushauri kutoka sehemu mbalimbali lakini nakuomba kitu kimoja kuwa makini sana katika ushauri ambao utakuwa unaupokea maana ushauri mwingine utapewa kwa lengo la kutaka kukubomoa hivyo kabla haujaukubali ushauri huo ufanyie tathimini na ujiridhishe ndipo uuchukue.

 Katika Safari ya kuelekea mafanikio hautakuwa peke yako Bali utakuwa na watu wengine na moja ya watu ambao utakuwa nao ni kama hao niliokutajia hapo juu. Lengo la kukubainishia makundi haya ni kukufanya uyajue makundi hayo ya watu na uchukue taadhari ya ni jinsi gani ya kukabiliana nayo.

Ni mimi rafiki yako
Baraka maganga

0754612413/0652612410.

Sunday, November 8, 2015

Tabia Hii Itakuweka Mbali Na Malengo Yako Na Kukufanya Usifanikiwe.


Kila mtu anataka kufanikiwa, hakika hakuna mtu asiyependa kufanikiwa. Lakini mafanikio hayaji hivi hivi mafanikio yanapitia mambo mengi sana yenye kufurahisha na yanayovunja  moyo. Lakini yote hayo hayatoshwi kukufanya usifanikiwe jambo jingine ambalo nalo litakufanya usifanikiwe katika safari yako ya kuyaelekea mafanikio ni ile tabia ya  kuwaendekeza marafiki.


 Kila mtu ana marafiki hilo halipingiki na sikatazi watu kuwa na marafiki lakini jambo ambalo nataka kukutaadharisha Leo hii ni kuwa tabia ya kuwaendekeza marafiki itakufanya usifanikiwe kabisa. Namaanisha nini kusema kuwaendekeza marafiki?. Kuwaendekeza marafiki ni pale ambapo unajikuta ukishindwa kufanya mambo yako na shughuli zako ulizojiwekea kisa marafiki wamekuja na kukushawishi ufanye jambo jingine ambalo ni kinyume na ratiba yako binafsi.

 Jiulize ndugu msomaji ni mara ngapi rafiki yako amekuwa akija na kukuomba mwende sehemu mkatembee, mkaangalie Mpira kwenye vibanda vya mpira, mwende kwenye kumbi za sinema au hata kwenda kubalizi ufukweni. Na ukamkubalia ili hali ulikuwa na shughuli zako ambazo ulipanga kuzitekeleza. Chukulia mfano umejiwekea malengo ya kupunguza uzito hivyo ukaweka ratiba ya kufanya mazoezi ili kutimiza lengo lako la kupunguza uzito, unapoanza tu kufanya zoezi anakuja rafiki yako na kukuomba mkaangalie mpira, nawe kwa kuwa umemwendekeza rafiki yako unaamua kuhairisha mazoezi na kuambatana nae kwenye kibanda cha mpira ili mkaangalie mpira. Sasa jiulize kwa kufanya hivyo utayatekeleza malengo yako kweli?.

 Jifunze kumkatalia rafiki yako kwa baadhi ya mambo Fulani Fulani ili tu uweze kutekeleza ratiba zako ulizojipangia. Hiyo haitapunguza urafiki wenu kama kweli mnapendana na nimarafiki haswa kwani nachoamini Mimi rafiki yako lazima awe mwelewa na mwenye kuzijua na kuziheshimu ratiba zako, pia asiyeweza kuzivunja ratiba zako ovyoovyo. Nawe inatakiwa uwe na uwezo wa kuitetea ratiba yako ambayo itakufanya utekeleze malengo yako. Usipende kumfurahisha rafiki yako wakati wewe unajiumiza Mara kwa Mara. Kuwa na rafiki haimaanishi umnyenyekee maana kufanya hivyo unaweza kujikuta umekuwa mtumwa na sio rafiki.

 Marafiki ni watu muhimu sana tena sana lakini ni watu wa kuwa nao makini kwa kuwa rafiki anaweza kuwa mtu wa kwanza kukuulia ndoto zako bila wewe kujua kuwa ni rafiki yako ndiye chanzo cha wewe kushindwa kutekeleza malengo yako jambo la msingi na kubwa la kufanya chunguza sana ratiba anazokuletea rafiki yako.

Ni mimi rafiki yako
Baraka maganga
Bmaganga22@gmail.com

0754612413/0652612410.

Saturday, November 7, 2015

Jifunze Kusema Hapana Kwa Makundi Haya Manne (4) Ya Watu.


 Kihistoria tumejenga utamaduni Fulani ambao binafsi naomba niuite utamaduni mbovu sana, utamaduni huo ni ule wa kukubali kila tunaloambiwa na watu ambao wapo juu yetu kiuwezo, kiumri hata kielimu. Utamaduni huu binafsi nauona kuwa muda mwingine huwa kikwazo kikubwa sana katika maisha yetu na hata kuua ndoto na malengo yetu. Leo ndungu msomaji nataka nikushauri haswa kwa wewe ambaye unataka mafanikio kuwa jifunze kusema hapana kwa watu wafuatao:-

 1. Wazazi, tumeaminishwa kuwa kuwakubalia wazazi kwa kila jambo ambalo wanatuambia na hicho ndio kipimo cha heshima na adabu ya mtoto kwa wazazi wake. Tumeaminishwa kuwa mtoto anayekubali kila analoambiwa na wazazi wake huyo ndio mtoto mtiifu. Lakini leo nakushauri jifunze kusema hapana kwa wazazi wako, hii haitakufanya uonekane mtoto asiye na heshima wala adabu na unaposema hapana sema hapana ukiwa na lengo la kutaka kutetea ndoto na malengo yako. Chukulia leo wazazi wanataka usome masomo ya sayansi ili uje kuwa daktari lakini wewe ukiangalia huyawezi hayo masomo, kwa kuogopa kusema hapana unakubali ili hali ulitaka kusoma masomo ya biashara matokeo yake unakuja kufeli na udakitari haupati. Wazazi wale wale wanaanza kukulaumu kwa kushindwa kuwaambia ukweli mwanzo na matokeo yake umefeli. Angalia ulivyojialibia leo hii lakini yote haya yametokana na wewe kushindwa kutamka neno hapana.

2. Rafiki, tumekuwa ni watu wa kukubaliana na marafiki zetu hata kwa mambo tusiyoyataka. Pengine tumekuwa tukifanya hivyo ili tu tuonekane marafiki wema na watii na wenyekujari ama tumekuwa tukifanya hivyo kwa lengo la kuogopa kuvunja urafiki wetu. Lakini kushindwa kusema hapana kwa marafiki zetu kumetuponza wengi sana  leo hii wengine wapo jera kwa kesi za kuiba, wengine ni vibaka, wengine wavuta madawa ya kulevya na wengine wamepoteza maisha yote haya ni kwasababu tulishindwa kusema hapana kwa marafiki zetu. Mwambie rafiki yako hapana pindi unapohisi anakushawishi ufanye mambo ambayo huyataki.

3. Ndugu,jiulize ni Mara ngapi unekuwa ukifanya mambo usiyoyapenda wala kuyataka kisa alikuambia kaka, dada, babu, bibi, mjomba, shangazi n.k. bila shaka jibu ni Mara nyingi. Jiulize tena kwanini nilifanya hayo mambo nisiyoyapenda ili hali nilijua siyapendi? Jibu ni kwasababu ulishindwa kusema hapana kwa kuwa uliogopa watakuona sio mtiifu tena mwenye kukosa adabu. Jiulize tena kama unataka kuendelea na tabia hiyo ya kushindwa kusema hapana. Natumaini jibu ni hautaki tena kuendelea maana umegundua kufanya hivyo kunakuweka mbali na malengo yako.

4. Viongozi wako wa dini, hawa ni watu ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana katika maisha yetu. Lakini tunachokosea ni kuwa tumewaamini sana hawa watu kiasi kwamba tumewafanya kuwa wao hawakoseagi hivyo badala ya kuwaheshimu tunawaogopa sana tukiamini woga wetu kwao ndio heshima kwao. Ndio maana hata ikitokea wanatuambia kitu ambacho hatukiitaji sisi hujikuta tumekikubali tu ili tuonekane watiifu kwao. Jifunze kusema hapana kwa watu hawa pia futa woga kabisa sema hapana kama kiongozi wako wa dini atakuambia vitu usivyovipenda.


 Kusema hapana kwa mtu aliye juu yako kiumri, uwezo, elimu, kiongozi wa dini au waalimu wako sio utovu wa nidhamu na tafadhari unaposema hapana hakikisha unatamka neno hili ukiwa na uhakika kuwa unasimamia ndoto na malengo yako usiseme hapana kisa umesoma hapa. Kabla hujasema hapana tafakari kwa kina sana ndipo useme hapana.
E

ndelea kutembelea mtandao huu kwa mambo mengi mazuri ya kujifunza na kujijenga. TWENDE SOTE.

Thursday, November 5, 2015

Sababu nne (4) zitakazokufanya ukate tamaa


.
Mara nyingi sana tukekuwa tukifanya shughuli zetu tukiwa na matumaini kuwa shughuli zetu zitafanikiwa lakini wakati mwingine mambo hutuendea kombo ambapo badala ya kufanikiwa katika zile shughuli zetu hujikuta tukiwa tumeshindwa. Pindi tunaposhindwa hapo ndipo ile hali ya kukata tamaa hujitokeza ambapo huwa tunakata tamaa. Sababu zinazotufanya tukate tamaa baada ya kushindwa ni pamoja na zifuatazo:-
1.woga, binadamu ni kiumbe ambaye amejawa na woga sana, kila binadamu ni mwoga lakini kinachowafanya wengine waonekane sio waoga wakati wengine wakionekana kuwa waoga sana no ule  uwezo wa kuukabili woga wao. Yule mwenye uwezo wa kukabiliana na hali ya woga huonekana kuwa sio mwoga ili hali yule asiye na uwezo wa kuukabili woga wake huonekana mwoga. Woga hutufanya tukate tamaa na tusijaribu tena pindi tunaposhindwa, hivyo ni vyema tujifunze  kukabiliana na woga.
2. Kutokuwa na malengo, tunakata tamaa kwasababu tunakuwa hatuna malengo, maisha bila malengo kwa binadamu hayana maana. Hii ni kwa kuwa binadamu asiye na malengo ni sawa na mnyama wa kufugwa ambaye kila siku hutegemea kupelekwa malishoni au kupelekewa chakula/malisho. Hivyo basi jiwekee malengo pia amua na kujitoa katika kuyatekeleza malengo uliyojiwekea, ukifanya hivyo hutoweza kukata tamaa tena.
3. Kutojiamini, pindi unaposhindwa unatawaliwa na hali ya kuto kujiamini ambapo muda mwingine hali ya kuto kujiamini huletwa na ile tabia ya kuanza kujilinganisha na wengine. Pindi unapojilinganisha na wengine hasa wale unaoamini wako juu yako kiuwezo hufanya ushindwe kujiamini katika shughuli zako na hivyo kukata tamaa yako. Ili ufanikishe jambo Fulani yapaswa ujiamini kuwa unauwezo wa kulifanya jambo hilo.
4. Kukosa uvumilivu, watu wengi tumekuwa tukikata tamaa pengine mapema zaidi hii ni kutokana na kukosa uvumilivu. Wengi wetu tumekuwa tukiamini mafanikio ni rahisi hivyo pindi tunapokumbana na vikwazo tunakuwa sio wavumilivu na matokeo yake tunakata tamaa mapema sana. Kukosa uvumilivu imekuwa sababu kubwa sana ambayo hutufanya tukate tamaa mapema bila hata kufikiri kujaribu kwa mara ya pili au hata ya tatu. Tujifunze kuwa wavumilivu katika safari ya mafanikio.
   Hauwezi kukipata kile unachokitaka ikiwa unakata tamaa, Leo hii watu wengi wamekuwa wakilalamika sana juu ya kutokufanikiwa kwao na wakati mwingine huwatupia lawama wengine lakini sababu ya kutokufanikiwa kwao hutokana na kukata tamaa kwao. Nimekueleza juu ya sababu zinazokufanya ukate tamaa ili uziepuke na hatimae ufanikiwe.

Funguo Tatu (3) Muhimu Za Kukuza Biashara Na Kuwa Yenye Mafanikio.


Kuna njia muhimu za kuikuza biashara yako katika namna ambayo itakupendeza na kukuridhisha, biashara ambayo itawafurahisha wateja wako, na kuweza kukupatia kipato unachokitaka. Zifuatazo ni funguo tatu  zitakazokusaidia kupata mafanikio ya kweli katika biashara na kuweza kuifanya biashara yako kuwa na ukuaji endelevu.

1. Kuwa kiongozi wa biashara yako.
Ili kuweza kujenga biashara yenye mafanikio na yenye ukuaji endelevu unahitaji kuwa kiongozi wa biashara yako, badala kuwa mfanya kazi tu katika biashara hiyo, jione kama kiongozi wa biashara yako. Anza kwa kuwa wazi kuhusu kwa nini umeamua kuanzisha au ulianzisha biashara yako, na vipi kuhusu maono yako, unataka nini kutoka kwenye biashara yako na kwa ajiri ya maisha yako. Waza na ufikiri kama kiongozi wa biashara, na ubakie  mwenye nguvu na mwenye hamasa kubwa ili uweze kuiongoza biashara yako katika mwelekeo ulio sahihi.

2. Weka umakini kwa wateja wako.
Wajue wateja wako, Jitumbukize katika matatizo yao, changamoto zao,  masuala yao na malengo yao ili uweze kujenga, kutoa bidhaa na huduma zenye kiwango kikubwa na zenye ubora kwa wateja wako. Kutoa huduma na bidhaa ambazo zitaweza kupata matokeo makubwa na kuleta majibu chanya kutoka kwao. Na kama mteja wako ataweza kufurahia huduma na bidhaa zako unazotoa, kwa kiasi kikubwa sana atakusaidia katika   kukuongezea wateja, na kipato kwenye biashara yako kitaongezeka ikiwa atawaambia wengine kuhusiana na huduma zako nzuri pamoja na bidhaa unazotoa.

3. Weka umakini katika biashara yako.
Unachopaswa kuzingatia hapa ni kufahamu mambo muhimu katika  biashara yako ( masoko, mauzo n.k.)  ili kuweza kuifanya biashara yako ifanye kile inachosema, kwa kufanya hivi utakuwa unaiweka biashara yako katika njia ya kuelekea kwenye mafanikio na ukuaji. Unahitaji kuwa na ufanisi katika maeneo muhimu ya biashara yako, kuwa na ufanisi katika masoko, uuzaji na utunzaji wa fedha za biashara na hata kwenye mambo ya sheria. inakupasa kujua wajibu wako kama mmiliki wa biashara, unapaswa kujua rasilimali muhimu zinazoitajiwa na biashara yako, ili uweze kuiendesha biashara yako vizuri na kuweza kukupatia faida.
Hizo ni funguo tatu za kujenga biashara yenye mafanikio na ukuaji endelevu, nakutakia kila la kheri katika kuanzisha, kuendeleza na kuboresha biashara yako. Endelea kutembelea mtandao huu kila siku kwa mambo mazuri ya kujifunza na kujihamasisha na pia harika na wenzako ili nao waweze kupata mambo haya mazuri.
Ni mimi rafiki yako.
Geofrey mwakatika.
0767382324/0675555987.