Habari ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa,
ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri katika kuhakikisha kuwa
unashughulikia ipasavyo yale unayo yahangaikia ili tu kujiletea mafanikio
ambayo ndio kila mtu anayoyahangaikia. Nami nikusihi kwa moyo mmoja kuwa
endelea kupambana mpaka uyatimize yale unayoyaamini kama mafanikio kwako.
Pambana pambana bila kuchoka na mafanikio utayaona tu.
Wakati unaendelea kupigana ili kuyasaka mafanikio
yafuatayo ni mambo saba muhimu ambayo nataka uyaepuke kwa hali na mali kama
kweli unataka kufanikiwa, ni muhimu ukayasoma mambo haya na kuyaweka akilini
mwako ili yakusaidia katika safari yako ya kuelekea mafanikio, mambo hayo ni
kama ifuatavyo:-
Epuka woga,
ndugu mpendwa msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa ni muhimu ukatambua
kuwa woga ni adui wa mafanikio, woga utakukwamisha sana tena sana hivyo basi
kama kweli unataka kufanikiwa acha kabisa kujenga woga juu ya yale mambo ambayo
unayataka au unataka kuyafanya. Njia moja wapo ya kuepuka woga juu ya kitu fulani
ni kwa wewe kufanya kile unachokiogopa zaidi na zaidi. Fanya kile unachokiogopa
na woga utaushinda kwa hakika.
2. Epuka wivu,
wivu hauwezi kukupeleka popote, na kwa mtu anaetaka kufanikiwa wivu hatakiwi
kuwa nao, kama kweli unataka kufanikiwa achana na habari zile za sijui wivu wa
maendeleo sijui nini. Kitu ambacho unatakiwa ukijue ndugu msomaji ni kuwa wivu
ni wivu tu achana na habari ya wivu wa maendeleo. Wivu utakuzuia kujifunza
kutoka kwa wale waliofanikiwa hivyo basi pingana na habari hizi za wivu na
badala yake acha kuwaonea wivu waliofanikiwa na nenda kajifunze kwao.
3. Epuka chuki, mtu
mwenye chuki hatofautiani sana na mtu mwenye chuki. Acha kujenga chuki na watu,
usitegemee kufanikiwa ikiwa una chuki moyoni mwako. Chuki juu ya wenzio
itakukwamisha maana chuki haina msingi wowote bali ni tabia ambayo ni maalumu
na mashuhuri kwa watu ambao hawaelewi ni nini haswa wanakitaka maishani. Hivyo
basi kama wewe unataka kufanikiwa basi achana na habari hizi za chuki.
4. Epuka kisasi, je
umekumbwa au unakumbwa na hali ya kisasi yaani unajisikia kulipiza kitu fulani
yaani kwamba ukiona mtu fulanii kakufanyia kitu fulani nawe unataka uje ulipize
hivyo hivyo. Haimaanishi kuwa mtu akikutendea mambo mabaya basi nawe uweze
kumlipizia mabaya hayo hayo. Usipoteze muda wako katika kufikiria juu ya ni
vipi ulipize kisasi kwa mwenzio bali tumia muda wako mwingi kuwaza utafanya
nini ili uweze kufanikiwa.
5. Epuka tamaa,
achana na habari ya tamaa, tamaa haina msingi wowote kwako kama kweli unataka
kufanikiwa. Tamaa ni kitu kibaya sana na ambacho hakiwezi kukufanya usonge
mbele, usipende kutamani tamani vitu ovyo badala yake jua jinsi ya kujizuia juu
ya matamanio yako. Usiwe mtu wa tamaa ambaye unataka kuwa ma kila kitu badala
yake kuwa na vitu vya msingi sio lazima uwe navyo vyote. Hivyo basi achana na
habari za tamaa.
6. Epuka hasira,
ikiwa unataka kufanikiwa ni vyema ukatambua kuwa hasira ni kitu kibaya sana. Ni
kweli kuwa kila mtu anahasira na viwango vya hasira vinatofautiana kutoka mtu
mmoja kwenda mtu mwingine. Nachotaka kukushauri ni kuwa jifunze kuzizuia hasira
zako. Ikiwa unataka kufanikiwa jifunze kuanzia sasa kuweza kuzizuia hasira zako,
hii itakusaidi wewe kuweza kufanya maamuzi yaliyo bora maana mara nyingi sana
watu tumekuwa tukifanya maamuzi kutokana na hasira alafu baadae tunakuja kuanza
kujuta, hii ni baada ya hasira yetu kuisha. Hivyo basi jifuze kuzizuia hasira
zako.
7. Epuka ushirikina,
wapo watu ambao huamini kuwa mafanikio huja kwa kuwa mshirikina, naomba nikuambie
kuwa haya ni mawazo ya kijinga na yasiyofaa katika ulimwengu wa sasa. Kama
kweli unataka kufanikiwa acha kabisa kutegemea habari za ushirikina.
Hayo ni mambo saba muhimu ambayo inabidi
uyaepuke ili uweze kufanikiwa. Epuka mambo haya kwa kuwa hayana msingi wowote
na wala hayawezi kukufikisha popote. Hivyo ndugu msomaji pigana uwezavyo
kuyaepuka mambo haya.
Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Wasiliana nami kwa.
Simu: 0754612413 au 0652612410.
Barua
pepe: Bmaganga22@gmail.com
No comments:
Post a Comment