Tuesday, November 10, 2015

Zijue Njia Sita (6) Za Kujifunza.


Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa. Kama ilivyokawaida kila tunapokutana hapa huwa tunakutana kwa lengo la kupeana maarifa mapya ambayo yatatusaidia na baadae kutuletea mafanikio.

 Baadhi tumekuwa tukiamini kuwa njia bora ya kujifunza ni ya  sisi kwenda shuleni kisha mwalimu anakuja anasimama mbele yetu na kuanza kutufundisha mambo mbalimbali. Wengi tunaamini kujifunza kupo shuleni tu. Kujifunza kwa njia ya shule ni njia ya hasili na njia hii hutufanya wakati mwingine tukose uelewa wa mambo ya msingi kuhusu maisha. Chukulia mfano wewe unaetegemea elimu ya kutoka shuleni utajifunzaje elimu kuhusu pesa maana shuleni hakuna somo la pesa. Sasa kama jibu ni huwezi kujifunza elimu ya pesa kutoka shuleni basi zijue njia nyingine zifuatazo ambazo zitakusaidi kujifunza mambo mengi sana tofauti na yale ya shuleni.

1. Kutazama, hii ni njia mojawapo ya kujifunza mambo mengi sana na jambo la kushangaza ni kwamba njia hii ni rahisi na haina gharama kubwa sana lakini ndio njia ambayo haitumiki na wengi.Njia hii ni nzuri sana maana inahusisha kutazama shughuli aifanyayo mtu Fulani kisha ukajifunza jambo. Mfano unaweza kumtazama fundi selemala jinsi anavyounganisha mbao mpaka kupata mlango hivyo ukawa umejifunza jambo Fulani na taratibu ukilifanyia kazi utajikuta nawe unauwezo wa kuunganisha mbao na kupata mlango kama alivyokuwa akifanya selemala uliyekuwa unamtazama. Hivyo basi jifunze kupitia njia ya kutazama.

2. Kusoma vitabu, vitabu vinasiri nyingi sana kuliko wengi wetu tunavyofikiri. Vitabu hivi daima huwa vinaandikwa na wataalamu na watu waliofanikiwa kimaisha ambapo huandika kwa lengo ya kufunza kuhamasisha, na kutia motisha maishani. Lakini kitabu cha kwanza katika kuhamasisha ni biblia kwa wakristo na kwa waislamu ni kuruani. Vitabu vimejaa mambo mengi ambayo huwezi kuyapata shuleni kama unavyotegemea, vitabu vimejaaa historia za watu waliofanikiwa, changamoto zao, maisha yao mpaka kufanikiwa na baada ya kufanikiwa. Pia kuna vitabu ambavyo vimejaaa elimu kuhusu pesa mfano wa kitabu hicho ni kitabu cha rich dad poor dad cha bwana Robert kiyosaki. Hivyo basi jenga utamaduni wa kujisomea angalau kitabu kimoja kwa wiki.

3. Video, Leo hii unaweza kujifunza mambo mbalimbali kupitia video za wataalamu mbalimbali. Leo hii kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia wataalamu wamekuwa wakifundisha mambo mbalimbali ambayo hurekodiwa na kuwekwa katika mitando kama vile YouTube ambapo unaweza kuzitazama video hizo na kujifunza. kama unahisi unaelewa zaidi kwa njia ya video kuliko zingine basi tumia njia hii ya video katika kujifunza kwako. Leo hii kuna baadhi ya mambo mfano kuhusu komputa unaweza kujifunza kwa kupitia kuangalia video fupi za YouTube.

4. Semina, hii ni njia nyingine ambayo kwa hapa kwetu Tanzania imeibuka hivi karibuni. Njia hii imeshika kasi sana na kuonekana ni bora sana na ni rahisi kwa kiasi Fulani. Semina zimegawanyika ambapo zipo semina za bure na za kulipia. Usiogope kutoa pesa na kwenda kwenye semina mbalimbali, Bali nakushauri tumia pesa yako katika semina na hautokuja jutia hilo. Nakuambia hivyo kwa kuwa Nina uhakika semina zinafundisha mambo mengi mazuri ambayo usingeweza kuyapata shuleni na kwingineko.

5. Kanda za kunasia sauti/ tepu rekoda, hii ni njia nyingine sawa na njia ya video ila tofauti ni kuwa video huhusisha sauti na picha ila njia hii haihusishi sauti na picha. Hivyo basi kama unahisi hauwezi kujifunza kwa kupitia njia ya video au kusoma vitabu maana kuna vitabu ambavyo huwekwa katika mfumo wa sauti(audibook) ambapo unaweza kuyapata Yale yaliyomo kwenye kitabu kwa njia ya kusikiliza.

6. Kuwauliza wataalamu. Kila unachotaka kujifunza kuna watu wanakijua na watu hawa ndio hufahamika kama wataalamu. Wataalamu hawa hawapo kwa ajili ya kujisifia au kusifiwa juu ya utaalamu wao Bali wapo ili kuwasaidia watu ambao wanashida na vitu ambavyo wao ndio wanautaalamu navyo. Unapotaka kujifunza jambo na ukahisi unahitaji ushauri wa kitaalamu basi fanya hivyo ili uweze kujifunza kupitia wataalamu hao.

 Nimekuorodhoshea njia hizo sita za kujifunza tofauti na shuleni. Simaanishi kuwa watu wasiende shuleni kujifunza Bali maana yangu ni kuwa watu wasitegemee shule pekee maana shule pekee haitoshi, hivyo watumie na njia hizi katika kujifunza Yale ambayo Nina uhakika shuleni hayapo mfano elimu juu ya pesa.

Ni Mimi rafiki yako
Baraka maganga.
Bmaganga22@ gmail.com.

0754612413/0652612410.

No comments:

Post a Comment