Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya
maarifa, ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri
kuhakikisha unayatekeleza yale uliyojiwekea na ikizingatiwa kuwa mwaka ndio huo
unakwenda mwishoni. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vyema kwa kuwa mungu
kakujalia afya njema na uzima. Tuendelee kuelimishana juu ya mambo mbalimbali
ambayo yatatufanya tuweze kuyafikia mafanikio. Leo nataka kukushirikisha jambo moja ambalo ni umuhimu
wa kujiuliza swali kwanini kwa kila unalolifanya.
Ndugu msomaji kumbuka siku zote kuwa ubongo wa mwanadamu
hukaa katika hali ya kufanya kazi pale unaposukumwa kutafuta majibu ya maswali
unayojiuliza kinyume na hapo akili hudumaa na kufanya ubaki kuwa vile vile, hii
ni sababu namba moja ya mimi kukuambia kuwa jifunze kujiuliza kwanini kwa kila
jambo unalolifanya. Sababu ya pili ni kwa kuwa utapata majibu ya yale uliyokuwa
huyajui. Pengine kuna kitu unakifanya au kuna hali uliyonayo lakini hujajua
haswa kwanini unayo hiyo hali husika, ndio maana nakusihi jiulie swali hili.
Kuna watu ni wavivu sana tena sana, yaani wao hawapendi
kufanya shughuli yoyote zaidi hutaka wao waletewe kila kitu. Daima watu hawa
huwa ni mabingwa wa kutazama runinga, kupenda kwenda sehemu za starehe. Kama
wewe ni mmoja wapo wa watu wa namna hiyo ulishawahi kujiuliza kwa nini wewe uko
hivyo?, ukijiuliza kwanini unaweza kupata majibu kuwa pengine ni mazingira au
ni katika hali ya kutaka kuiga vitu ili kuonekana ni mwenye kwenda na wakati.
Majibu utakayo yapata yatakusaidia kubadili hali husika kama utakuwa hauipendi
hali hiyo.
Wewe ulie mlevi, ulishawahi kujiuliza kwanini umechagua na
kuyafata maisha ya kunywa pombe na kulewa kila siku?, kwanini unafanya hivyo
ili hali unajua madhara yaletwayo na ulevi wa kupindukia?, je ulishawaza
itakuwaje ukiacha pombe?, kwanini unang`ang`ania pombe? , kwanini hutaki
kuacha?. Ukijiuliza maswali juu ya tabia yako hii na kama kweli huipendi
unaweza kujinasua katika mtego huu.
Wewe ulie mnene na hauufurahii unene wako je ulishawahi
kujiulia kwanini unanenepa nenea ovyo? Pengine unene wako unatokana na kula
sana vyakula vyenye mafuta alafu hutaki kufanya mazoezi ili kuyapunguza mafuta
hayo. Kwanini unaendelea kula vyakula vinavyokufanya unenepe ovyo wakati unajua?
Na kwanini hutaki kuacha?
Mifano hapo juu mitatu nimeiweka kama baadhi ya tabia tu
ambazo wengi tunazo na hatujui pengine ni kwanini tunapenda kuwa hivyo.
Nimeweka mifano ya matendo au tabia mbaya haimaanishi kuwa kwa zile tabia nzuri
haupaswi kujiuliza swali la kwanini bali nazo unapaswa kujiuliza lakini
nimeweka tabia hizo kwasababu inawezekana ndizo zinazotusumbua sana wengi wetu
na kutufanya tusiweze kusonga mbele hivyo basi kwa kujiulia swali kwanini
tunaweza kupata majibu ambayo yatatusaidia kufanya uamuzi wa ni namna gani tunaweza kuziacha
tabia hizo mbaya.
Kwa ile nzuri tunapaswa kuwa na majibu pia ya kwanini
tunafanya hivyo kwa sababu kuna muda tabia au matendo yetu mazuri yanaweza
kuwafurahisha watu hivyo wakaja kutuomba ushauri lakini hii ikiwa ni katika hali ya kutaka kujifunza
kutoka kwetu wanaweza kutuuliza swali la kwanini tunafanya hivyo. Mfano
unapenda sana kujisomea vitabu mbalimbali unaweza kuulizwa kwanini unafanya
hivyo?, swali hili litakuwa jepesi ikiwa ulishatangulia kujijibu mwenyewe
kwamba kwanini unafanya kitu husika. Lakini kama hukuwahi kufanya hivyo
itakusumbua sana.
Naamini kuwa kila jambo lina sababu yake ya kufanyika hivyo
kwa kila unalolifanya tafuta sababu ya wewe kufanya hivyo haijalishi jambo hilo
ni zuri au ni baya jambo la msingi kwako ni kujiuliza tu kwanini unafanya hivyo
ili kuiamusha akili yako ambapo kwa lile jambo zuri itaamuka na kulifanya zaidi
na zaidi na hivyo utapiga hatua kubwa sana katika hilo.
Ewe ulie mwalimu, dereva, daktari, kondakita, mjasiriamali,
mchungaji, nesi, padre, sheikh, msanii, mwinjilisti, mlokole, mpagani, mchawi,
mfanyabiashara, muongo, mzinzi, mlevi, mwamasishaji, mwandishi, mcheza soko,
mwajiliwa n.k. ulishawahi kujiuliza kwanini unafanya au umechagua hilo
unalolifanya sasa?.
Ni mimi rafiki yako
Baraka maganga.
0754612413/0652612410.
asante
ReplyDelete