Tuesday, December 29, 2015

Acha Kuangalia Matawi Pekee Kama Kweli Unataka Kufanikiwa.


Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa, ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri kuhakikisha unayatekeleza yale uliyojiwekea na ikizingatiwa kuwa mwaka ndio huo unakwenda mwishoni. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vyema kwa kuwa mungu kakujalia afya njema na uzima. Tuendelee kuelimishana juu ya mambo mbalimbali ambayo yatatufanya tuweze kuyafikia mafanikio. Leo tena tumekutana hapa katika hali ya kuendelea kupeana maarifa mapya na leo nataka uelewe juu ya jambo hili moja ambalo nalo ni kuachana na tabia ya kuangalia matawi pekee kama kweli unataka kufanikiwa.

Najua kila mtu anaifahamu miti na kama kila mtu anaifahamu miti sina haja ya kueleza zaidi kuwa mti una nini na nini. Kimsingi mti unaweza kuwa na sehemu nyingi sana lakini mimi ntauangalia mti katika sehemu mbili ambazo ni mizizi na matawi. Mizizi ni sehemu ya chini kabisa ya mti ambayo hukua kuelekea chini, na matawi ni sehemu ya juu ya mti ambayo hutawanyika katika pande mbalimbali za dunia na wakati mwingine hutupatia kivuli kizuri.
Matawi ni nini basi maishani au katika mafanikio haswa?, au kuangalia matawi ni nini haswa?. Napo sema acha kuangalia matawi pekee kama kweli unataka kufanikiwa namaanisha kuwa acha ile tabia ya kuamini kuwa maisha yamejaa raha tu, na kama ni katika biashara acha ile hali ya kuangalia faida tu bila kuangalia hasara. Au kwa kifupi usitegemee raha tu maishani, na katika biashara nyingi sana watu wamekuwa wakiangalia faida peeke bila kujali hasara. Hapa ndipo naposema acha kuangalia matawi pekee.
Nitajikita zaidi katika biashara,biashara nyingi sana zimekuwa zikianzishwa nyingi nyingi mno lakini kati ya hizo ni biashara chache zimekuwa zikifanikiwa sababu kubwa nayo iona ni ile tabia ya kutegemea faida tu wakati wote. Takwimu zinaonesha kuwa kati ya biashara kumi ambazo huanzishwa basi ni biashara tatu au mbili ndizo hudumu zingine zote saba au nane hufa baada ya muda mfupi. Biashara nyingi zinazoazishwa hazidumu kwa sababu wafanyabiashara wengi wanaoanzisha biashara hizo wanauelewa mdogo juu ya biashara husika ndio maana wao hulenga tu katika faida na sio hasara, wao huwa hawaelewi kuwa kuna kitu hasara katika biashara ndio maana hata inapotoke hasara ndogo tu hawawezi kumudu na matokeo yake biashara zao hupeperushwa na upepo na kuwaacha watupu na huo ndio huwa mwisho wao.
Uimara wa matawi hutokana na uimara wa mizizi yake yaani kama mti ni dhaifu katika mizizi yake basi hata matawi yake yatakuwa dhaifu na kinyume chake.  Leo hii mtu anapokuuliza juu ya biashara fulani yeye hukuuliza swali moja tu vipi biashara hii inalipa? Akiambiwa ndio inalipa yeye hukurupuka mara moja na kujiiingiza katika biashara bila hata kufanya uchunguzi wa kina swala yeye amejua kwa kuchukua bidhaa, gharama ya usafirishaji na bei ya kuuzia basi anajiingiza katika biashara  husika bila hata kujali taarifa zingine.
Biashara nzuri inamtegemea sana mfanyabiashara yaani ujuzi na uwajibikaji wa mtu husika katika biashara husika ndivyo viikuzavyo biashara kinyume cha hapo biashara haiwezi kukua yaani ikiwa mfanyabiashara anaujuzi mdogo basi hata biashara yake itakuwa ya kawaida. Biashara za siku hizi sio zile zenye kufanya kwa mazoea au kuiga zinahitaji muda mwingi kujifunza ili kuzielewa vizuri sio kuingia kichwa kichwa maana ukiingia kichwa kichwa kesho tu utakuwa nje kwa kuwa hujajipanga.
Mfanyabiashara bora na mzuri ni yule mwenye uwezo, ujuzi, na elimu juu ya biashara husika sio elimu ya darasani   bali elimu ya juu ya biashara husika. Mfanya biashara mzuri ni yule anayejua kama kuna faida basi kuna hasara hivyo huanza kuandaa mikakati ya atafanyaje pindi swala la hasara litakapo tokea na sio Yule anaewaza faida tu muda wote huyu ni yule anayeangalia matawi tu bila kujali mizizi na huyu hatodumu muda mrefu katika biashara bali atafirisika mapema.
Jifunze kuangalia mizizi kabla ya matawi japo matawi ndio huonekana kiurahisi. Yaani jifunze kutafuta chanzo cha tatizo fulani kabla ya kuanza kulaumu au kupiga makelele ovyo na kuanza kulaumu. Jifunze kuchunguza jambo kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake sio unachunguza katikati na mwisho kama kweli unataka kufanikiwa.
Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.

0754612413/0652612410.

1 comment:

  1. katika hili nimejifunza kitu maana mm nilikuwa nawaziz faida tu kuofikiri npale nitakapo kumbana na hasara nitafanyaje nashukuru nimejifunza kufanya uchunguzi makini kabla y kuanzisha bihashara

    ReplyDelete