Monday, December 28, 2015

Jiulize Swali Hili Kwa Kila Unalolifanya.


Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa, ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri kuhakikisha unayatekeleza yale uliyojiwekea na ikizingatiwa kuwa mwaka ndio huo unakwenda mwishoni. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vyema kwa kuwa mungu kakujalia afya njema na uzima. Tuendelee kuelimishana juu ya mambo mbalimbali ambayo yatatufanya tuweze kuyafikia mafanikio. Leo nataka  kukushirikisha jambo moja ambalo ni umuhimu wa kujiuliza swali kwanini kwa kila unalolifanya.


Ndugu msomaji kumbuka siku zote kuwa ubongo wa mwanadamu hukaa katika hali ya kufanya kazi pale unaposukumwa kutafuta majibu ya maswali unayojiuliza kinyume na hapo akili hudumaa na kufanya ubaki kuwa vile vile, hii ni sababu namba moja ya mimi kukuambia kuwa jifunze kujiuliza kwanini kwa kila jambo unalolifanya. Sababu ya pili ni kwa kuwa utapata majibu ya yale uliyokuwa huyajui. Pengine kuna kitu unakifanya au kuna hali uliyonayo lakini hujajua haswa kwanini unayo hiyo hali husika, ndio maana nakusihi jiulie swali hili.
Kuna watu ni wavivu sana tena sana, yaani wao hawapendi kufanya shughuli yoyote zaidi hutaka wao waletewe kila kitu. Daima watu hawa huwa ni mabingwa wa kutazama runinga, kupenda kwenda sehemu za starehe. Kama wewe ni mmoja wapo wa watu wa namna hiyo ulishawahi kujiuliza kwa nini wewe uko hivyo?, ukijiuliza kwanini unaweza kupata majibu kuwa pengine ni mazingira au ni katika hali ya kutaka kuiga vitu ili kuonekana ni mwenye kwenda na wakati. Majibu utakayo yapata yatakusaidia kubadili hali husika kama utakuwa hauipendi hali hiyo.
Wewe ulie mlevi, ulishawahi kujiuliza kwanini umechagua na kuyafata maisha ya kunywa pombe na kulewa kila siku?, kwanini unafanya hivyo ili hali unajua madhara yaletwayo na ulevi wa kupindukia?, je ulishawaza itakuwaje ukiacha pombe?, kwanini unang`ang`ania pombe? , kwanini hutaki kuacha?. Ukijiuliza maswali juu ya tabia yako hii na kama kweli huipendi unaweza kujinasua katika mtego huu.
Wewe ulie mnene na hauufurahii unene wako je ulishawahi kujiulia kwanini unanenepa nenea ovyo? Pengine unene wako unatokana na kula sana vyakula vyenye mafuta alafu hutaki kufanya mazoezi ili kuyapunguza mafuta hayo. Kwanini unaendelea kula vyakula vinavyokufanya unenepe ovyo wakati unajua?  Na kwanini hutaki kuacha?
Mifano hapo juu mitatu nimeiweka kama baadhi ya tabia tu ambazo wengi tunazo na hatujui pengine ni kwanini tunapenda kuwa hivyo. Nimeweka mifano ya matendo au tabia mbaya haimaanishi kuwa kwa zile tabia nzuri haupaswi kujiuliza swali la kwanini bali nazo unapaswa kujiuliza lakini nimeweka tabia hizo kwasababu inawezekana ndizo zinazotusumbua sana wengi wetu na kutufanya tusiweze kusonga mbele hivyo basi kwa kujiulia swali kwanini tunaweza kupata majibu ambayo yatatusaidia kufanya  uamuzi wa ni namna gani tunaweza kuziacha tabia hizo mbaya.
Kwa ile nzuri tunapaswa kuwa na majibu pia ya kwanini tunafanya hivyo kwa sababu kuna muda tabia au matendo yetu mazuri yanaweza kuwafurahisha watu hivyo wakaja kutuomba ushauri lakini  hii ikiwa ni katika hali ya kutaka kujifunza kutoka kwetu wanaweza kutuuliza swali la kwanini tunafanya hivyo. Mfano unapenda sana kujisomea vitabu mbalimbali unaweza kuulizwa kwanini unafanya hivyo?, swali hili litakuwa jepesi ikiwa ulishatangulia kujijibu mwenyewe kwamba kwanini unafanya kitu husika. Lakini kama hukuwahi kufanya hivyo itakusumbua sana.
Naamini kuwa kila jambo lina sababu yake ya kufanyika hivyo kwa kila unalolifanya tafuta sababu ya wewe kufanya hivyo haijalishi jambo hilo ni zuri au ni baya jambo la msingi kwako ni kujiuliza tu kwanini unafanya hivyo ili kuiamusha akili yako ambapo kwa lile jambo zuri itaamuka na kulifanya zaidi na zaidi na hivyo utapiga hatua kubwa sana katika hilo.
Ewe ulie mwalimu, dereva, daktari, kondakita, mjasiriamali, mchungaji, nesi, padre, sheikh, msanii, mwinjilisti, mlokole, mpagani, mchawi, mfanyabiashara, muongo, mzinzi, mlevi, mwamasishaji, mwandishi, mcheza soko, mwajiliwa n.k. ulishawahi kujiuliza kwanini unafanya au umechagua hilo unalolifanya sasa?.
Ni mimi rafiki yako
Baraka maganga.

0754612413/0652612410.

1 comment: