Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya
maarifa, ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri
kuhakikisha unayatekeleza yale uliyojiwekea na ikizingatiwa kuwa mwaka ndio huo
unakwenda mwishoni. Ni matumaini yangu kuwa unaendelea vyema kwa kuwa mungu
kakujalia afya njema na uzima. Tuendelee kuelimishana juu ya mambo mbalimbali
ambayo yatatufanya tuweze kuyafikia mafanikio. Leo tena tumekutana hapa katika
hali ya kuendelea kupeana maarifa mapya na leo nataka uelewe juu ya jambo hili
moja ambalo nalo ni kuachana na tabia ya kuangalia matawi pekee kama kweli
unataka kufanikiwa.
Najua kila mtu anaifahamu miti na kama kila mtu
anaifahamu miti sina haja ya kueleza zaidi kuwa mti una nini na nini. Kimsingi
mti unaweza kuwa na sehemu nyingi sana lakini mimi ntauangalia mti katika
sehemu mbili ambazo ni mizizi na matawi. Mizizi ni sehemu ya chini kabisa ya
mti ambayo hukua kuelekea chini, na matawi ni sehemu ya juu ya mti ambayo
hutawanyika katika pande mbalimbali za dunia na wakati mwingine hutupatia
kivuli kizuri.
Matawi ni nini basi maishani au katika mafanikio haswa?,
au kuangalia matawi ni nini haswa?. Napo sema acha kuangalia matawi pekee kama
kweli unataka kufanikiwa namaanisha kuwa acha ile tabia ya kuamini kuwa maisha
yamejaa raha tu, na kama ni katika biashara acha ile hali ya kuangalia faida tu
bila kuangalia hasara. Au kwa kifupi usitegemee raha tu maishani, na katika
biashara nyingi sana watu wamekuwa wakiangalia faida peeke bila kujali hasara.
Hapa ndipo naposema acha kuangalia matawi pekee.
Nitajikita zaidi katika biashara,biashara nyingi sana
zimekuwa zikianzishwa nyingi nyingi mno lakini kati ya hizo ni biashara chache
zimekuwa zikifanikiwa sababu kubwa nayo iona ni ile tabia ya kutegemea faida tu
wakati wote. Takwimu zinaonesha kuwa kati ya biashara kumi ambazo huanzishwa
basi ni biashara tatu au mbili ndizo hudumu zingine zote saba au nane hufa
baada ya muda mfupi. Biashara nyingi zinazoazishwa hazidumu kwa sababu
wafanyabiashara wengi wanaoanzisha biashara hizo wanauelewa mdogo juu ya
biashara husika ndio maana wao hulenga tu katika faida na sio hasara, wao huwa
hawaelewi kuwa kuna kitu hasara katika biashara ndio maana hata inapotoke
hasara ndogo tu hawawezi kumudu na matokeo yake biashara zao hupeperushwa na
upepo na kuwaacha watupu na huo ndio huwa mwisho wao.
Uimara wa matawi hutokana na uimara wa mizizi yake yaani
kama mti ni dhaifu katika mizizi yake basi hata matawi yake yatakuwa dhaifu na
kinyume chake. Leo hii mtu anapokuuliza
juu ya biashara fulani yeye hukuuliza swali moja tu vipi biashara hii inalipa?
Akiambiwa ndio inalipa yeye hukurupuka mara moja na kujiiingiza katika biashara
bila hata kufanya uchunguzi wa kina swala yeye amejua kwa kuchukua bidhaa,
gharama ya usafirishaji na bei ya kuuzia basi anajiingiza katika biashara husika bila hata kujali taarifa zingine.
Biashara nzuri inamtegemea sana mfanyabiashara yaani
ujuzi na uwajibikaji wa mtu husika katika biashara husika ndivyo viikuzavyo
biashara kinyume cha hapo biashara haiwezi kukua yaani ikiwa mfanyabiashara
anaujuzi mdogo basi hata biashara yake itakuwa ya kawaida. Biashara za siku
hizi sio zile zenye kufanya kwa mazoea au kuiga zinahitaji muda mwingi
kujifunza ili kuzielewa vizuri sio kuingia kichwa kichwa maana ukiingia kichwa
kichwa kesho tu utakuwa nje kwa kuwa hujajipanga.
Mfanyabiashara bora na mzuri ni yule mwenye uwezo, ujuzi,
na elimu juu ya biashara husika sio elimu ya darasani bali
elimu ya juu ya biashara husika. Mfanya biashara mzuri ni yule anayejua kama
kuna faida basi kuna hasara hivyo huanza kuandaa mikakati ya atafanyaje pindi
swala la hasara litakapo tokea na sio Yule anaewaza faida tu muda wote huyu ni
yule anayeangalia matawi tu bila kujali mizizi na huyu hatodumu muda mrefu
katika biashara bali atafirisika mapema.
Jifunze kuangalia mizizi kabla ya matawi japo matawi ndio
huonekana kiurahisi. Yaani jifunze kutafuta chanzo cha tatizo fulani kabla ya
kuanza kulaumu au kupiga makelele ovyo na kuanza kulaumu. Jifunze kuchunguza
jambo kuanzia mwanzo wake mpaka mwisho wake sio unachunguza katikati na mwisho
kama kweli unataka kufanikiwa.
Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
0754612413/0652612410.
katika hili nimejifunza kitu maana mm nilikuwa nawaziz faida tu kuofikiri npale nitakapo kumbana na hasara nitafanyaje nashukuru nimejifunza kufanya uchunguzi makini kabla y kuanzisha bihashara
ReplyDelete