Thursday, April 14, 2016

Sababu Za Kwanini Kila Siku Wewe Hauna Muda.

Habari za wakati huu ndugu msomaji wa makala za mtandao huu, ni matumaini yangu kuwa hu mzima na unaendelea vyema katika kubambana ili kuhakikisha kuwa unajiboresha zaidi na zaidi na baadae unaweza kukamilisha yale ambayo umekwisha kujiwekea kama malengo katika maisha yako. Nami nikusihi kuwa endelea kupambana pasipo kuchoka kwani harakati na mapambano yanaendelea kila siku.
Wakati unaendelea kupambana leo kuna jambo ambalo nataka kukushirikisha hapa, mambo yenyewe ni juu ya ile kauli ambayo tumekuwa wengi wetu tukiitumia ama kwa kupenda kuiga au hata kwa kutumia tu kwa sababu tumejizowesha kufanya hivyo. Kauli hii ni ya kusema sina muda. Hebu hapo hapo ulipo jiulize ni mara ngapi umekuwa ukijiambia kuwa sina muda pindi unaposhirikishwa jambo fulani iwe biashara, iwe semina, iwe kusoma kitabu n.k

Sasa kama unakumbwa na kauli hii basi leo nipo hapa ili kukupa sababu na namna ya kufanya ili uweze kuondokana na kauli hii maana imekuwa ikituferisha wengi wetu siku hadi siku.

1.      Kukosa  ratiba,ratiba ni mpangilio wako wa namna utakavyoianza siku na kuimaliza siku yako.  Kila mtu huianza ratiba yake kwa namna yake ya kipekee na kila mtu huianza ratiba yake pindi tu anapoamka kutoka kitandani. Ratiba huwa ni mpangilio wa mambo na shughuli ambazo utazitenda kuanzia unaanza siku mpaka unaimaliza, na hii huwa inakwenda sambamba na malengo yako. Sasa swali la kujiuliza ni kuwa wewe unaratiba?, kumbuka waswahili husema “mazoea hujenga tabia” nami nakuambia ratiba hujenga mazoea na ni kitu muhimu sana kwako wewe mwanamafanikio. Mfano nikuulize una muda maalumu wa kulala au huwa unalala tu pale unapohisi kulala. Ni muhimu ukajiwekea ratiba, hii itakusaidia wewe kupata muda wa ziada ambao huo unaweza kuutumia katika shughuli au mambo mengine unayoshirikishwa na unasema hauna muda. Anza na ratiba rahisi sana leo jiwekee muda maalumu wa kulala na muda maalumu wa kuamka alafu ndio zifuate ratiba zingine. Fanya hivyo kwa muda wa wiki mbili kwa nidhamu ya hali ya juu ndipo uanze kuongeza ratiba zingine.

2.      Umeshindwa kutenga muda wa uzalishaji na muda wa kupumzika, muda mwingine kutokana na kukosa ratiba tumekuwa tukijikuta kuwa tunashindwa kutenga muda wa kuzalisha na muda wa kupumzika. Hii ni hatari maana binadamu hutakiwa kupumzika maana yeye sio mtambo ambao umesetiwa ili kufanya kazi kila muda, kila dakika, kila sekunde hapana. Leo hii anza kwa kutenga muda wa kazi na muda wa kupumzika na katika muda wa kupumziki ndipo unaweza kuweka mambo mengine au shughuli ambayo ni rahisi ambayo haihitaji nguvu nyingi wala kutumia akili nyingi mfano mazoezi ya mwili. Kumbuka muda wa kupumzika uwe mchache kuliko muda wa kufanya kazi.


3.      Haujafanya maamuzi, wakati mwingine shida sio kuwa hauna muda ila shida ni kuwa haujafanya maamuzi ya kufanya kile unachoambiwa kufanya. Na kwa kuwa haujafanya maamuzi juu ya lile yaani wewe ulishaipanga akili yako kuwa kwa kila jipya ntakalo ambiwa mimi jibu langu liwe sina muda. Hii ni kukosa maamuzi na pia vile vile kukosa maamuzi hutokana na sababu kuwa hauna maamuzi yako binafsi bali unaishi kwa kufuata maamuzi ya wenzio tu jambo hili ni hatari sana. Sasa leo hii fanya maamuzi mapya ya kutafuta muda kwa kila unaloshirikishwa leo hii utenge muda wa kulifanya.
Ni jambo la ajabu leo hii kusema kuwa hauna muda wa kufanya jambo fulani tena lenye tija katika maisha yako mfano kwenda kwenye semina, kwenye mazoezi, kwenye makongamano ya kidini, kwenye mikutano ya kijasiriamali, au hata kusoma kitabu. Lakini una muda wa kuangalia TV kuanzai asubuhi hadi jioni. Au una muda wa kuingia na facebook na instgram kulike picha za wenzio tu.

                                             Mwandishi: Baraka Maganga.

     Mawasiliano:-simu-0754612413/0652612410.


                                                      :-barua pepe -Bmaganga22@gmail.com

No comments:

Post a Comment