Duniani kuna vitu vingi sana ambavyo binadamu huwa
tunakuwa tunavifanya au tunataka kuvifanya, vitu hivi vinaweza kuwa vizuri au
vibaya kutoka kwa mtu mmoja mpaka mtu mwingine hii ni kutokana na tofauti za kimtazamo
miongoni mwetu binadamu. Lakini pamoja na tofauti hizi za kimtazamo huwa
tunakuwa na kitu kimoja ambacho kinaweza kutuunganisha na kutuweka pamoja na
kitu hiki ndicho ambacho wapaswa kujua na kwenda nacho kama unataka kupata
matokeo makubwa. Kitu hicho sio kingine bali ni kanuni.
Nafahamu kanuni sio jambo geni sana kwako ndugu msomaji.
Kwa wale ambao wamebahatika kupita katika shule kuna masomo kama hisabati na
fizikia mfano haya ni masomo yenye kutawaliwa na kanuni, yaani katika utafutaji
wa majawabu ya maswali ya hesabu kuna kanuni na ukienda kinyume na kanuni hiyo
hauwezi kupata jibu mwafaka la swali lako. Mfano katika hisabati kuna kanuni
maarufu sana ijulikanayo kama MAGAZIJUTO. Hii kanuni ni kifupi cha baadhi ya
matendo mfano MA- husimama kwa niaba ya mabano wakati GA- husimama kwa niaba ya
gawanya. Hivyo katika kufanya swali la mtindo huu lazima uanze na kuzitoa namba
katika mabano, uje ugawanye, baadae uzidishe, ujumlishe na hatimaye utoe. Hivyo
ndivyo kanuni isemevyo na kwa kufanya hivyo basi utapata jibu sahihi kinyume na
hapo hupati jibu.
Sasa kama ilivyo katika hesabu hata katika maisha halisia
haya mambo yako hivyo hivyo. Maishani kila kitu kina kanuni zake leo hii
ukitaka kulima nyanya, kilimo hiki cha nyanya kina kanuni zake, ambazo lazima
uzifuate kwa makini na kama inavyotakiwa ndipo utapata mazao bora. Ukitaka
kulima miti lazima ujue kanuni za miti, mfano miti mingi huwa tayari kwa
kuvunwa baada ya kipindi cha miaka kuanzia mitano na kuendelea hiyo ni kanuni
ambayo unatakiwa uifuate kinyume na hapo hauwezi kupata kitu chochote kutoka
katika miti. Kwahiyo katika kilimo mfano jambo nalo taka kusisitiza ni kuwa
kila zao lina utaratibu wake ambao ni muhimu sana kwa nza sio muhimu ni lazima
ufuatwe na anaefanya kilimo husika, na ikumbukwe kuwa tofauti za mazao zinaleta
tofauti za kanuni ndio maana kanuni za miti huwezi kupeleka kwenye nyanya au
pilipili hoho.
Mafanikio ni kitu ambacho kina kanuni nyingi sana tena
sana, mfano wa kanuni hizo ni kama vile jiwekee malengo, usikate tamaa, kuwa na
marafiki chanya, fanya mazoezi ili kuimarisha afya ya mwili wako, tafuta timu
sahihi ya kushirikiana nayo, kuwa mvumilivu, ua hofu,kuwa na msimamo,epuka
visingizion.k.
Pengine umezoea kanuni haziko katika maandishi yaani
umezoea kanuni huwa zinakuwa katika mfumo wa namba, sikulaumu hii ni kutokana
na mfumo wa elimu ambao umepitia ambapo kila kanuni huwa ipo katika mfumu wa
namba, lakini kumbuka kuwa kule ni shuleni na hapa tunazungumzia maisha halisi
hivyo sio lazima kanuni hizi ziwe katika mfumo wa namba. Katika maisha halisi
kanuni nyingi zipo katika mfumo wa maandishi na ninaposema kanuni simaanishi
mtu mpaka uambiwe hii ndio kanuni hapana bali nacho rejelea hapa ni ile hali
hata ya kupewa utaratibu au maelezo ya jinsi gani ya kulifanya jambo hicho ndicho
nacho maanisha napo sema kanuni.
Swali la kujiuliza leo ni kuwa je unazijua kanuni za
unachokifanya? Kama jibu ni ndio je unazifuatata? Kama hauzifuati basi
nakuambia leo hiyo ndio sababu namba moja ya kwanini haufanikiwi. Na kama
huzijui unasubiri nini? anza kuzitafuta kuanzia leo hii.
Mwandishi:
Baraka Maganga.
Mawasiliano:-simu-0754612413/0652612410.
No comments:
Post a Comment