Monday, March 21, 2016

Jambo Hili Halitakusaidia Lolote Maishani.

Habari za wakati huu ndugu mpendwa msomaji wa  makala za mtandao huu, ni matumaini yangu kuwa hu mzima na unandelea vizuri katika kupambana zaidi na zaidi ili tu kuhakikisha kuwa unajiletea mafanikio ambayo umeyakusudia maishani. Nami nasema vizuri na endelea kupambana zaidi na zaidi bila kuchoka kwani mafanikio ndio kila kitu ambacho mtu anakitaka maishani hivyo ni haki yako wewe kupambana ili kuhakikisha unayapata mafanikio.Ni wengi sana ambao tumekuwa tukipigana kwa hali na mali katika kuhakikisha kuwa tunajiletea mafanikio, hili ni jambo ambalo huwa tunalifanya wengi wetu na tumekuwa tukilifanya kwa muda mrefu. Ni vizuri sana  kufanya hivyo binafsi huwa nafarijika sana napowakuta vijana wenzangu wanazungumzia mafanikio na wanapambana ili kujiletea mafanikio kama unafanya hivyo naomba pokea pongezi zangu. Hongera hongera sana.

Leo nataka kuzungumzia swala moja ambalo linaweza kukufanya usifanikiwe na ndio maana kichwa cha makala hii kinasema jambo hili halitakusaidia lolote. Jambo lenyewe ni kuwa na mtazamo hasi juu ya watu waliofanikiwa. Nimeamua kulizungumzia hili kwa kuwa kumekuwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa na mtazamo mbovu juu ya watu waliofanikiwa mfano wanawachukia watu waliofanikiwa, wanawaona kama ni watu wachoyo, wabinafsi, walaghai, wanyanyasaji na wenye tamaa za pesa kuliko watu wengine.
Pengine unasababu zako za kukufanya uwachukulie watu wenye mafanikio kwa namna ambayo unawachukulia hivi sasa, lakini naomba nikuambia haya kuwa kwanza pole sana kwa kuwatazama watu waliofanikiwa katika mtazamo hasi, pili naomba nikuambie kuwa siujali ukubwa wala udogo wa sababu inayokufanya wewe kuwachukia watu waliofanikiwa ila nachotaka kukuambia ni kuwa unachofanya sio sahihi. Sio sahihi kwa sababu haupaswi kufanya hivyo badala yake unatakiwa kuwachukulia watu walio fanikiwa kama darasa na waalimu wako.

Hakika kama unataka kufanikiwa hakikisha kuwa unajenga uhusiano mzuri na walio fanikiwa na kubwa jenga mtazamo chanya juu yao. Waone kuwa ni kama watu ambao ndio nyenzo muhimu ambazo unaweza kuzitumia na ukafanikisha mambo yako kwa kiasi kikubwa. Ukiwachukia watu wenye mafanikio ni dhahiri kuwa hata mafanikio nayo utayachukia, japo unaweza kujifariji kuwa mi nawachukia tu wenye mafanikio ila mafanikio nayapenda huko ni kujidanganya kwa hali ya juu yaani unahisi upo sahihi kwa mwonekano wa nje lakini ndani yake umejiharibia kila kitu.

Wachukulie watu wenye mafanikio kama darasa kwako, wachukulie kama watu ambao unaweza kuwa tumia kama daraja la kuweza kukuvusha wewe toka hapo ulipo na kukupeleka kule unako kutaka. Ukiwa na mtazamo chanya juu ya watu wenye mafanikio  hii itakusaidia wewe kuweza kuwafuata na kuweza kujifunza mambo mengi kutoka kwao tena kwa kiasi kikubwa.


Jambo la msingi ambalo unatakiwa ulijue kuanzia sasa na ulifahamu kwa asilimia zote ni kuwa mafanikio huja kwa kujifunza kutoka kwa walio fanikiwa sasa kama unawachukia watu wenye mafanikio hii inamaanisha nini, hii inamaanisha kuwa hutoweza kujifunza kutoka kwao, na kama ukishindwa kujifunza kutoka kwao maana yake utajifunza kutoka kwa walioshindwa na kama ukijufunza kutoka kwa walioshindwa basi na wewe utashindwa tu.

Hakuna sababu ya kuwachukia waliofanikiwa bali jambo ambalo wewe unatakiwa kufanya ni kuwapenda na kutaka kujifunza zaidi kutoka kwao, hii ndio njia ambayo inaweza kukufanya wewe kuwa mwenye mafanikio makubwa kama wao.

Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Waweza wasiliana nami kwa nambari za simu
0754-61-24-13 au 0652-61-24-10.
Au kwa barua pepe
Bmaganga22@gmail.com 

No comments:

Post a Comment