Thursday, February 11, 2016

Usiishi Ni Kama Hakuna Maisha Tena.


Katika maisha yetu sisi wanadamu tumekuwa tukiishi na watu wa aina tofauti tofauti kitabia, kimaumbile na kihali mbalimbali. Yote haya ni maisha tu
na tunaendelea kuishi katika hali hizi hata kama ikitokea kuwa zinatuletea shida lakini huwa tunajitahidi sana kukabiliana nazo ili tu kutaka kuhakikisha kuwa mambo yanaenda sawa. Haya ndio maisha yetu na huu ndio uhalisia wa maisha yetu yaani hatuwezi kufanana kwa kila kitu maishani.
Leo sasa nataka kukutahadharisha ndugu msomaji wa makala hii kuwa usihishi ni kama hakuna maisha tena, hapa nacho maanisha ni kuwa usihiishi ni kama leo ndio mwisho wako wa kuishi. Binadamu tunaishi tukiwa na matumaini kuwa kesho tutafika hilo ni jambo jema sana kwetu kwa kuwa na imani kuwa kesho tutaiona na ndio maana huwa tunajiwekea malengo ya siku, wiki, mwezi, nusu mwaka na hatimaye tunaweka malengo ya mwaka na hatimaye miaka.  Haya ni mambo ambayo wanadamu tumekuwa tukiyafanya mara kwa mara na kila siku aidha kwa kujua au kuto kujua ila ni dhahiri kuwa huwa tunayafanya mambo haya.Leo nataka nikuonye na kukutaadharisha wewe unayeishi ni kama kesho haitafika yaani unaishi ni kama unakufa leo. Kuna watu wanatabia hii usinishangae ni kama naongea mambo ambayo hayapo na kama bado hujanipata endelea kusoma utanielewa tu. Kuna baadhi ya matendo ambayo unaweza kuyatenda na hatimaye tafsiri yake ikawa ni kuwa unaishi ni kama hakuna maisha tena au ni kama kesho haifiki matendo hayo ni kama yafuatayo:-

Kuto kuweka akiba, kuna watu wanaishi pasipo kuweka akiba maishani mwao yaani yeye kwa kila pesa anayoipata au kitu anachokipata ana tumia chote bila kujua kesho itakuwaje. Maishani ni muhimu kujiwekea akiba, kama unatokea kwenye familia za wakulima utakuwa unaelewa fika sana maana ya kuweka akiba, mkulima baada ya mavuno lazima ataweka akiba ya chakula, nyingine kwa ajili ya kuuza na mgawanyo utaweza kuendelea. Kwanini mkulima huyu anaweka akiba ya chakula  na hasemi tutumie mazao yote?, ni kwasababu anajua kuwa kesho ipo ndio maana anaweka. Wewe ni mfanyakazi ukipata mshahara unatumia wote kiasi kwamba hata ukipata ugonjwa huwezi kujitibu hii ni hatari sana kwa maisha yako. Jifunze kuweka akiba maana itakusaidia hapo baadae. Weka akiba usitumie kila kitu ni kama unakufa leo leo. Wakati nikiwa mtoto mdogo niliwahi kusimliwa na mzee mmoja kuwa kuna mtu baada ya mavuno ya mahindi yake, alikula chakula akashiba na hatimae akahisi kuwa kutokana na alivyoshiba hana haja ya kula tena maishani, hatimaye akaamua kuchoma kihenge chake, lakini kilichomkuta ni kuwa kabla hata kihenge kile hakijaisha njaa tayari ilikuwa ishamuuma sana. Na hakuweza kupata tena chakula. Yeye alihisi maisha yanaishia pale ila maisha yaliendelea. Wakati ule nikiwa mtoto stori hii ilikuwa ya kufurahisha tu lakini leo ina funzo kuwa ni muhimu kujiwekea akiba maishani usihishi ni kama kesho haipo.

Kuwadhurumu watu, kuna watu ni maarufu wa tabia hii lakini wewe unayefanya hivi tambua kuwa sio kila siku utadhurumu alafu unaweza kuwa ulishawahi kuwadhurumu watu wako wa karibu na hatimaye ukawa umepoteza uaminifu kwa ndugu zako hao na hatimaye hata siku ukija kupata shida wakashindwa kukusaidia kitu kutokana na tabia yako ya kuwadhulumu.

Kusema uongo, watu wenye tabia hii nao wanaingia hapa katika wale wanaoishi ni kama kesho haipo, hawa huendelea na tabia yao ya kudanganya lakini wakishazoeleka watu hupoteza uaminifu kabisa kwao, kuna stori moja juu ya kijana mmoja ambaye alikuwa mchugaji wa mbuzi katika kijiji kimoja ambacho kilikuwa jirani na mbuga za wanyama, kijana huyu alizoea kuwadanganya wanakijiji kwa kupiga kelele za chui kutaka kuwashambulia mbuzi wake hivyo kelele zake zilikuwa ni zile za kuhitaji msaada lakini mara kwa mara wanakijiji walipofika walikuta hakuna chui na kijana huyo alikuwa akiwacheka wanakijiji hao na kujiona mjanja hivyo wanakijiji walizoea kuwa huwa anasema uongo. Siku ya siku alipiga kelele kumbe siku hiyo chui alikuja kweli na kutokana na uongo wake kuzoeleka hakuna mwanakijiji aliyekuja kumsaidia na hatimaye mbuzi wake wakaliwa na chui. Hii ni kwa kuwa alijenga mazoea ya kuwadanganya wanakijiji, kijana huyu aliishi ni kama hakuna kesho. Alihisi uongo wake utaendelea kila siku lakini kumbe haikuwa hivyo maana siku hiyo chui alitokea na asijue cha kufanya.

Usipende kufanya mambo ni kama unakufa leo au ni kama yesu anarudi leo na kuja kuwachukua watu wake bali ishi huku ukiwaza kuwa kesho ipo hivyo ujinga, uongo, uzembe na kitu chochote kisicho na maana kinaweza kukuletea shida kesho na ukashindwa kutatua au ukajikuta upo matatani kutokana na kuishi ni kama maisha yanaishi  leo leo.
Ni mimi rafiki yako,

Baraka Maganga.
Wasiliana nami kwa nambari za simu 0754612413/0654612410 au kwa barua pepe:- Bmaganga22@gmail.com.


No comments:

Post a Comment