Tuesday, February 16, 2016

Usifanye Kwa Kuwa Umeona Wanafanya.







Umekuwa ukitaka kufanya jambo au mambo mbalimbali maishani au umekuwa ukitaka kufanya mambo mbalimbali. Lakini wakati
hujafanya jambo husika ni muhimu ukajiuliza kwa nini unafanya au unataka kufanya. Mara nyingi sana watu wamekuwa wakifanya vitu kwa kukurupuka sana yaani wao hufanya tu kwa sababu wameona mtu fulani anafanya kile kitu. Maisha hayahitaji maswala ya kukurupuka. Yaani usiwe mtu wa kukurupuka na kuona kuwa hili linawezekana bali kuwa na mipango katika mambo yako.






Leo hii ukizungumzia biashara, biashara nyingi sana zinakufa kwa sababu watu wanakurupuka yaani mtu anatoka huko bila hata kufanya uchunguzi wa biashara husika na kujilizisha ndipo aianze ila yeye anakurupuka na kuanza tu biashara. Huko nyuma nilishawahi kuonya juu ya kufanya biashara sababu inalipa nikasisitiza kuwa kabla hujafanya biashara fanya uchuguzi juu ya upatikianaji wa bidhaa, usafirishaji wake, pamoja na gharama za usafirishaji na vile vile swala la soko yaani ni vipi bidhaa yako inauzika na ni wapi zaidi bidhaa yako inaweza kuuzika kiurahisi kuliko sehemu nyingine. Hayo ndio baadhi ya mambo ambayo biashara inahitaji, usiwe mtu wa kukurupuka na kuingia katika biashara bila hata uchunguzi wowote ule.

Leo hii kila mtu utasikia nataka kuwa mjasiriamali lakini chunguza kati ya hao wanaosema wanataka kuwa wajasiriamali ni wangapi wanafanikiwa. Leo hii mtu akimwendea mjasiriamali aliyefanikiwa kuwa ulianzaje anzaje mpaka ukafika hapo, labda akajibiwa kuwa nilikuwa mwajiriwa na baadae niliacha kazi na kujiiingiza katika ujasiriamali rasmi. Kwa kuwa amejibiwa hivyo aendelei kuuliza zaidi ili apate taarifa zaidi na zaidi lakini kwa kuwa yeye ni mkurupukaji basi anabeba wazo kuwa ili niwe mjasiriamali lazima niache kazi, ndugu yangu, ndugu yangu kuwa makini sana tena sana maana ujasiriamali sio kuacha kazi tu na hapo hapo unakuwa mjasiriamali. Unapotaka kuwa mjasiriamali fanya uchunguzi wa kutosha maana taarifa moja haikutoshi kuna mambo unahitaji kuwa nayo ili kuwa mjasiriamali bora na sio vinginevyo hivyo basi kuwa makini usiwe mkurupukaji wa mambo na kuanza tu pasipo uchunguzi
.
Njoo katika ndoa za siku hizi, leo hii kuna ndoa nyingi sana zinafungwa kweli kweli, tena kwa bwebwe nyingi sana tena sana lakini chunguza katika ndoa hizo zinazofungwa leo hii au siku hizi ni ngapi zinadumu?. Utagundua kuwa ni chache sana na kama ukitaka kwenda mbele zaidi kuwa kwanini hazidumu ni kwasababu wanaofunga ndoa hizi wengi wanakurupuka  tu na kufunga ndoa hizo. Leo hii watu wanaoa au kuolewa tu kwa sababu wameona wengine wanafanya hivyo au kwa sababu baba alioa na mama nae aliolewa na baba basi nami lazima nioe au niolewe, watu hawa huwa wanafanya hivyo bila hata kuangalia ndoa hizi zilifungwa katika mazingira gani na waliofunga ndoa hizo walijipanga vipi mpaka kuzikamilisha hakuna hilo wao huamua tu kufunga ndoa husika bila hata kufanya tathimini ya kutosha sasa huku ni kukurupuka kwa kiwango cha juu.

Kimsingi maishani huitaji kukurupuka na kufanya mambo ya ajabu ajabu au maamuzi ya ajabu ajabu bali inatakiwa ufanye uchunguzi wa hali ya juu ukijiridhisha na hapo ndipo ufanye hilo unalotaka kulifanya na sio unatoka tu huko kisa umeona jambo fulani linafanyika basi nawe unalifanya bila uchunguzi.

Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
Wasiliana nami kwa nambari za simu 0754612413/0654612410 au kwa barua pepe:- Bmaganga22@gmail.com.


No comments:

Post a Comment