Tuesday, January 26, 2016

Ni Muda Wa Kuachana Nazo Sasa

.
Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea kupambana kwa hali na mali ili tu uweze kufanikisha yale ambayo umekuwa ukiyahangaikia mara kwa mara. Vizuri endelea kupambana naama hakuna kitu cha bure hapa duniani, maana hata miujiza huja kwa wale ambao huwa wanakuwa wakiitafuta miujiza hiyo. Sio waliokaa tu wakisubiri miujiza hivyo nakusihii endelea kupambana ndugu msomaji wa mtandao huu.


Je unakumbwa na wasiwasi wa kufanikiwa kutokana na historia yako ya nyuma zile kauli wanazokuambia wanaokuzunguka zinakurudisha nyuma katika hali ya kutaka kusonga mbele katika kuhakikisha kuwa unafanikiwa katika maisha yako. Je? unajua ni kwa nini kauli ulizopandikizwa kutoka utotoni  zinaendelea kukurudisha nyuma katika safari yako ya kuyaelekea mafanikio, ni kwasababu umeziamini na kuzifanya kuwa ukweli wako. Sasa jiambie mwenyewe kuwa ni wakati wa kuachana nazo sasa.

Zile imani ulizojijengea zamani ya kuwa hutofanikiwa na kuwa tajiri kwa kuwa wazazi wako ni masikini, imani ya kuwa huto fanikiwa kwa kuwa wazazi wako ni masikini, ni muda wa kuachana nazo maana hazina msingi wowote na wala hazikujengi wala kukusaidia chochote bali zinakudidimiza zaidi na zaidi badala yake wewe pambana kweli kweli hata kama unatokea katika familia masikini, na mafanikio utayaona tu, maana wapo waliokuwa kama wewe na waliotokea chini kama wewe na wakafanikiwa hivyo hilo lisikupe shide sana bali achana na hiyo imani.

Uliambiwa kuwa wewe ni mjinga na hauwezi chochote na mwalimu wako, ni wakati wa kuachana na kauli hii ambayo ulikuwa umeiamini kwa kuwa ilitoka kwa mwalimu wako na kupitia kigezo cha sifa ya ualimu basi ukaamini kuwa hauto fanikiwa fanya kama Thomas Edison ambaye pamoja na kukataliwa na walimu watatu tofauti kuwa hafai kuwa mwanafunzi wa kujifunza chochote lakini alijifunza na kuwa mwanasayansi mkubwa duniani na mpaka leo anaheshimika kama mwanasayansi mashuhuri duniani. Hii ni kutokana na sababu kuwa yeye aliachana na kauli za waalimu wake, hivyo basi hata wewe unaweza kufanya hivyo na ukafanikiwa pia, hivyo achana na kauli mbovu alizokuambia mwalimu wako.

Walikuita mbumbumbu mtaani kwenu, mtaani kwenu wewe ndio ulionekana kuwa mtoto mbumbumbu kuliko wote na ukafutwa kabisa kwenye watoto ambao wanaweza kuleta mabadiliko yoyote au kuleta mafanikio yoyote ambayo yataisaidia jamii yako na wewe ukaamini kuwa kweli hauwezi kutokana na maneno yao. Ni muda sasa wa kuachana na kauli hizo ambazo hazina msingi wowote bali ni za ukatishaji taama.

Lazima utambue kuwa  tunakuwa kadri tunavyofikiri, hata bibilia imeliandika hilo kuwa kadri ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo huwa. Hii inamaana kuwa wewe mwenye ndiye mwamuzi wa maisha yako yaani ni kadiri unavyojiona wewe mwenyewe ndivyo huwa unakuwa. Na biblia haijasema kadri wamwonavyo watu ndivyo mtu huwa, hilo ni jambo ambalo halijaandikwa wala kusemwa. Hivyo basi kama wamesema hauwezi kufanikiwa ni wao na sio wewe, wewe usizifuate kauli zao ambazo hazina msingi wowote bali wewe endelea kushikilia ukweli ambao unauona nafsini mwako na katika kuushikilia ukweli huu uwe ni ukweli ule ambao ni  chanya achana na kauli hasi kabisa maana hazikufikishi popote.

Kumbuka nimesema ni muda wa kuachana nazo zile kauli zote ambazo ni hasi, ni muda wa kuachana nazo maana hazina msaada kwako ila zina kudumaza na kukudidimiza zaidi na zaidi. Na kubwa zaidi juu ya kauli chanya ni kuwa haziwezi kukuletea mafanikio yoyote.

Twende sote.

Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Wasiliana nami kwa.
 Simu: 0754612413 au 0652612410.
Barua pepe: Bmaganga22@gmail.comNo comments:

Post a Comment