Wednesday, January 27, 2016

Hivi Ndivyo Mambo Yatakavyokuwa Baada Ya Wewe Kufanya Kitu Hiki Kimoja.


Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea kupambana kwa hali na mali ili tu uweze kufanikisha yale ambayo umekuwa ukiyahangaikia mara kwa mara. Vizuri endelea kupambana naama hakuna kitu cha bure hapa duniani, maana hata miujiza huja kwa wale ambao huwa wanakuwa wakiitafuta miujiza hiyo. Sio waliokaa tu wakisubiri miujiza hivyo nakusihii endelea kupambana ndugu msomaji wa mtandao huu.


Mafanikio yanahitaji ahadi ndugu mpendwa msomaji wa makala hii. Hili ni jambo ambalo ningependa uweze kulifahamu kuanzia sasa,kuwa mafanikio yanahitaji ahadi. Yaani baada ya kujiwekewa malengo unapaswa sasa kuweka ahadi juu ya utekelezaji wa malengo yako. Pengine umekuwa ukijiwekea ahadi bila kujua ahadi ni kama pale unaposema kuwa nataka kupunguza uzito likiwa kama lengo lako sasa pale unaposema lazima kila siku nifanye mazoezi kwa muda wa nusu saa, tayari hapo unakuwa umejiwekea ahadi katika maisha yako. Au unasema nataka kuamka kila siku saa kumi na moja alfajiri ili niweze kufanya shughuli zangu za ndani kabla ya kwenda katika mihangaiko yangu, kuamka saa kumi na moja ni ahadi tayari uliyokwisha jiwekea katika maisha yako.

Tumekuwa watu wa kujiwekea ahadi nyingi nyingi tena ahadi zingine zinakuwa kubwa na zenye kututisha kiasi kwamba tunaweza kufikiri kuwa hatutoweza kutimiza ahadi hizo. Kimsingi ahadi na malengo ni vitu ambavyo vinaenda sambamba na vinaweza kukupatia shida katika kuvitofautisha lakini tofauti ni kuwa malengo yanaanza alafu ndio ahadi hufata. Sasa kwa kuwa ahadi ni hatua moja wapo katika kuyaelekea mafanikio basi ni vyema ukatambua kuwa yafuatayo ni mambo ambayo yatakukumba baada ya kuwa umejiwekea ahadi zako wewe mwenyewe:-

1.    Vikwazo vitaibuka, baada ya kuwa umeshajiwekea ahadi zako vikwazo vitaibuka sana tena vingi kuliko unavyodhani. Vitaibuka vikwazo vya aina mbili ambavyo ni vikwazo vya nje na vya ndani. Vikwazo vya nje ni vile ambavyo vitatokana na wale watu wanaokuzunguka kama vile marafiki, ndugu au hata wazazi, ambao wanaweza kukuzuia wewe katika kuweza kutekeleza ahadi yako, zinaweza zikawa kauli zao juu ya ahadi yako au hata kukucheka na kukupinga zaidi na zaidi. Vikwazo vya ndani ni vile ambavyo unajiwekea mwenyewe kama vile uvivu, kukosa umakini, kupuuzia ahadi yako n.k. hivyo vikwazo vyote hivi visikutishe katika kuweza kuishikiria ahadi yako na hatimaye kuweza kuitekeleza ipasavyo.

2.    Utafanya makosa, katika kuelekea kutekeleza ahadi yako utafanya makosa kadha wa kadha, makosa haya yapo ili tu kukufunza. Kama unataka kufanikiwa ni lazima uwe na mtazamo tofauti juu ya makosa unayoyafanya. Kama kweli unataka kusonga mbele katika safari yako ya mafanikio sasa ni wakati wa kubadili mtazamo wako katika makosa unayoyafanya. Amini kuwa makosa yapo tu ili kuweza kukufunza na sio kingine. Hivyo basi usirudi nyuma katika kuitekeleza ahadi yako uliyojiwekea, makosa yasikutishe bali jifunze jifunze kutokana na makosa.


3.    Utavunjwa moyo, hili nalo litakukumba kwa kiasi kikubwa na hasa kitakacho kuvunja moyo ni pale utakapo kuja kujikuta umefanya makosa mengi na pale utakapo ona kuwa unakumbwa na vikwazo vingi sana. Mambo haya yote yanaweza kukuvunja moyo  kwa kiasi kikubwa sana, lakini kwa wewe unae yasaka mafanikio kamwe usivunjike moyo bali wewe endelea kuishikiria ahadi yako.

Tambua kuwa haya yote ni majaribu ambayo dunia itakuwekea ili kukupima ni jinsi gani uko makini juu ya ahadi yako. Mara nyingi watu wengi hutamani kuachana na ahadi zako, lakini wewe unaye yasaka mafanikio hutakiwi, hutakiwi kukata tamaa kamwe. Kama alivyosema bwana winstone Churchill “never never never give up” au kama alivyosema bwana james .J. Gorbelt “you become a champion by fighting one more round, when things are tough you fight one more round”. Yaani unakuwa mshindi baada ya kupambana hatua moja zaidi na zaidi hata kama mambo yakiwa magumu pambana hatua moja zaidi.
Twende sote.

Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Wasiliana nami kwa.
 Simu: 0754612413 au 0652612410.
Barua pepe: Bmaganga22@gmail.com


No comments:

Post a Comment