Wednesday, January 13, 2016

Ifahamu Njia Ya Kutumia Ili Kupanga Shughuli Zako Katika Vipaumbele.

Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri katika kuyatekeleza majukumu yako ya kila siku. Nami nasema vizuri endelea kupambana mpaka uyatekeleze yale uliyokwisha kujiwekea.
Wakati unaendelea kupambana ili kuhakikisha kuwa unafanikiwa, wapo watu ambao wanahisi kuwa wanashughuli nyingi sana na hawajui ni ipi shughuli waanze nayo. Ikiwa unaona au kuhisi kuwa unashughuli nyingi sana na haujui ni ipi sahihi kuanza nayo basi hapa nakuletea njia sahihi ya kutumia ili uweze kujua ni shughuli ipi ya kuanza nayo, njia yenyewe inaitwa ABCDE. Hii ndiyo njia yetu ya kuweza kukusaidia kupanga shughuli zako. Ntaifafanua njia hii kama ifuatavyo:-,





Shughuli A- shughuli ya kuwa katika kundi hili inapaswa kuwa shughuli ya muhimu sana, hapa kinapaswa kuwa kitu cha muhimu sana ambacho ni lazima ukifanye au kifanyike. Shughuli ambayo inapaswa kuwa na jina la A ni lazima utambue kuwa ni shughulia ambayo isipofanyika basi ina madhara makubwa sana. Mfano wewe ni mfanyabiashara na unaitegemea biashara husika katika kuendesha maisha yako basi hiyo shughuli ndio inapaswa kuwa hapo, maana kwanza ni muhimu, lazima ufanye ili uishi na mwisho ukiacha kufanya basi madhara yapo.
Shughuli B- hii ni shughuli ambayo inatakiwa uifanye, shughuli ambayo inatakiwa iwepo hapa ni ile ambayo pia isipofanyika ina madhara lakini sio muhimu sana kama ilivyo katika shughuli A. mfano kama umeamua kuanzisha program ya kufanya mazoezi kila siku asubuhi kabla ya kuelekea katika shughuli zako ni muhimu ukafanya hivyo ingawa kuto kufanya kuna madhara ya kuwa afya yako itadhoofika lakini sio muhimu sana maana wapo ambao hawafanyi zoezi na afya zao ni nzuri tu.
Shughuli C- katika kundi hili linapaswa kuwa na shughuli ambayo ni vizuri ifanyike lakini haina madhara yoyote. Mfano kuamua kwenda kuwatembelea ndugu mahali fulani kama vile dada, kaka, shangazi, bibi au babu, ukitazama vizuri swala la kwenda kuwatembelea ndugu mara kwa mara ni vizuri lakini hakuna madhara yoyote makubwa. Au shughuli nyingine ni kama vile kwa mfanyakazi ambae anataka kwenda kunywa chai au kula chakula pahali fulani na wafanyakazi wenzake, ni vizuri kufanya hivyo lakini kuto fanya hivyo hakuna madhara makubwa. Au kwa yule aliyeoa ni vizuri kupiga simu kuulizia leo mkeo kapika nini lakini hakuna madhara yoyote usipo fanya hivyo. Hivyo basi shughuli zote zenye kufanana na hizo zinapaswa kuwa hapa katika kundi hili.
Shughuli D- hapa pana husisha shughuli yoyote ile ambayo unaweza kumwachia mtu aifanye.  Ni muhimu utambue kuwa yakupasa uyaache yale ambayo yanaweza kufanywa na mtu fulani ili ayafanye yeye badala yako. Hii itasaidia nini haswa?, hii itakusaidia wewe kuokoa muda ambao ungeupoteza kufanya jambo ambalo linaweza kufanywa na mtu mwingine. Mfano mama mwenye binti zake wakubwa nyumbani anapaswa kuwaachia shughuli kama vile za usafi wa nyumba na yeye akawahi katika shughuli zake kama vile biashara zake.
Shughuli E- hapa ni shughuli ambazo unaweza kuamua kutokuzifanya kabisa. Hizi ni shughuli ambazo unaweza kuamua kuzifanya au kutokuzifanya na hazina madhara yoyote. Mfano shughuli ya kujibu kila jumbe au  kila unachokiona katika makundi ya whatsapp.
Mara nyingi sana watu huwa tunakabiliwa na changamoto pale ambapo tunapaswa kufanya jambo fulani, hii ni kutokana na kuwa na shughuli nyingi sana ambazo tunaamini kuwa zote ni za muhimu, utakuta mtu anataka kwenda kwenye biashara, mara kufanya zoezi, mara kwenda kumtembelea shangazi n.k. huyu ni mtu mmoja ambae anataka kuyafanya yote haya na hajui aanze na lipi. Kama unakubwa na shida hizo basi dawa ndiyo hiyo nimekupatia.  

Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Wasiliana nami kwa.
 Simu: 0754612413 au 0652612410.
Barua pepe: Bmaganga22@gmail.com





No comments:

Post a Comment