Tuesday, January 19, 2016

Chagua Timu Sahihi Ya Kushirikiana Nayo.


Habari ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa, ni matumaini yangu kuwa unaendelea vizuri katika kuhakikisha kuwa unashughulikia ipasavyo yale unayo yahangaikia ili tu kujiletea mafanikio ambayo ndio kila mtu anayoyahangaikia. Nami nikusihi kwa moyo mmoja kuwa endelea kupambana mpaka uyatimize yale unayoyaamini kama mafanikio kwako. Pambana pambana bila kuchoka na mafanikio utayaona tu.

Katika maisha yetu sisi  wanadamu tumekuwa tukijikuta tunaunda timu ya watu ambao tunakuwa tunashirikiana nao mara kwa mara. Najua kila mtu atakuwa na timu ya kushirikiana nayo yaani una watu wako wa karibu ambao mara kwa mara umekuwa ukishirikiana nao kufanya nao mambo mbalimbali. Hili ni jambo ambalo kila binadamu huwa analifanya kila siku na kila wakati. Sina shida na hilo ila shida iliyopo ni aina ya watu ambao tunashirikiana nao.

 Je tunawafahamu ipasavyo hawa watu ambao tumekuwa tukishirikiana nao mara kwa mara katika mambo yetu yawe ya muhimu na yale yasiyo ya muhimu. Kama unataka kufanikiwa maishani hakikisha kuwa unashirikiana na watu ambao ni sahihi na munaendana nao, sisemi  kuwa lazima muwe mnaendana kielimu, kiumri, urefu na rangi za mwili lakini jambo la msingi ni kule kuendana kimtazamo na mawazo.

Mafanikio yanahusisha sana fikira yaaani fikira zako ndizo hukuletea mafanikio au kuto kukuletea mafanikio. Mwenendo wa fikira zako ndio ambao huamua wewe uwe wapi. Ndio maana kama unataka kuwa mwenye mafanikio basi hakikisha kuwa unazichunguza kwa kiwango kikubwa sana fikira zako. Na kama unataka kutoka kule uliko kwenda mbele zaidi yaani kwenye mafanikio  basi hakikisha kuwa una badili fikira zako kama ulikuwa na fikira mbovu kuhusu maisha, mafanikio, utajiri na umiliki mali basi anza kuzibadili na ukishazibadili nenda mbali zaidi kwa kutafuta timu sahihi ya kushirikiana nayo.

 Ni muhimu ukatambua kuwa ndugu msomaji mafanikio huendana sana na watu ambao unashirikiana nao. Wazungu wana msemo usemao kuwa “birds of feather floks tugeza” kwa tafsiri sisi tunaweza sema ndege wenye mabawa hutembea pamoja. Msemo huu unamaana sana na kama kweli unataka kufanikiwa basi hakikisha kuwa msemo huu unakukaa kichwani na haukutoki kamwe, yaani ufanye msemo huu kama kichochea chako cha kuelekea mafanikio.

Msemo huu unauhalisia mkubwa sana maishani hebu yachunguze makundi mbalimbali ya watu hata hapo mtaani kwako na kwingineko, waangalie watu ambao huwa wanashirikiana je wanaendana au huwa hawaendani?, waangalie walevi au watu wanaokunywa pombe huwa wanakuwa wanafahamiana na huwa hata wana namna yao ya kuwasiliana na wewe ambaye sio mlevi unaweza ukapata shida kuwaelewa hii ni kutokana na lugha yao, waangalie vijana wa kijiweni, waangalie walokole, waangalie watu wanaopenda michezo n.k.

Leo hii ni ngumiu kumkuta mlokole aliekomaa kijiweni akishirikiana na vijana hao wa kijiweni, au ni vigumu sana kumkuta mlevi amekaa na mtu ambayehatumii pombe wala kilevi cha aina yoyote ile. Sasa unajua kwanini watu hawa huwa wanachagua watu wanao endana nao, ni kwasababu wanajua kupitia watu hao watapata mawazo na fikira zenye kuendana nao. Yaani watakuwa wakibadilishana mawazo yao juu ya yale ambayo wanayafanya.

Sasa kwa kupitia mifano ya watu hawa ambao nimekuwekea hapo juu basi nawe unaetaka kufanikiwa hakikisha unajipatia timu sahihi ya kushirikiana nayo, timu hii itakuwa chachu ya mafanikio yako, maana utapata mawazo mbalimbali, utapata changamoto mbalimnbali ambazo zitakufanya uwe bora zaidi na zaidi na uweze kusonga mbele.
Kama kweli unataka kufanikiwa hakikisha unakuwa na fikira chanya na fikira chanya ndio utazipata kutokana na watu ambao unashirikiana nao. Watu wapo tu shida ni kuwa wewe ukoje kama unamtazamo chanya basi utafanya mambo chanya na utapata watu wenye fikira chanya hivyo ni wewe tu na sio kuwa huwezi kupata watu, watu wapo tu.

Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Wasiliana nami kwa.
 Simu: 0754612413 au 0652612410.
Barua pepe: Bmaganga22@gmail.comNo comments:

Post a Comment