Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona
ya maarifa, ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri
katika mapambano yako na kuhakikisha mwisho wa siku unafika kule ulikokuwa unahitaji
kufika. Nami nasema usikatetama wala kurudi nyuma kwani mapambano yanaendelea.
Binadamu tumekuwa watu wa kufanya makosa mbalimbali,
ambapo mengine huwa tunayatenda ama kwa kujua au kuto kujua. Yote kwa yote ni
katika mfumo wa maisha kwa kuwa kuna usemi wa kiingereza usemao “we learn
through mistakes and those who never commit mistakes they never learn” ukiwa na
maana kuwa tunajifunza kupitia makosa na yule asiyefanya makosa hajifunzi.
Nianzie hapa kauli imesema tunajifunza kupitia makosa hii haina maana kuwa
ufanye kosa makusudi alafu useme
najifunza. Kauli hii haswa ipo kwa lengo la kutuhamasisha kuwa tuwe watu wa
kujaribi tena tusiwe watu wa kuogopa kujaribu kisa tunahofia kushindwa au
kufanya makosa maana tunajifunza kupitia makosa.
Ulishawahi kuambiwa kuwa fanya kitu fulani kisha ukatoa
jibu kuwa siwezi bila hata kuthubutu kujaribu?, mara ngapi umekuwa ukiwasihi
ndugu, jamaa, marafiki na watu wengine wa karibu nawe kuwa wafanye jambo fulani
wakakujibu pale pale pasipo hata kufanya tathimini ya kile unachowaambia
wakatoa jibu la kuwa hawawezi. Kauli ya siwezi imekuwa kauli maarufu na naiona
ikishika kasi sana miongoni mwa watanzania. Na hili ndio kosa ambalo wengi
tumekuwa tukilifanya ama kwa kujua au kuto kujua. Kama ulikuwa hujui hili ni
kosa leo nakuambia hili ni kosa tena kosa kubwa sana ambalo unalifanya. Unaweza
kujiuliza kivipi si nasema ukweli kuwa siwezi kwa mambo ambayo naamini siwezi
au mbona hili kwangu mimi najua haliwezekani ndio maana nimesema siwezi n.k.
baada ya hapo ukaongeza na swali kuwa kivipi sasa nasema unafanya kosa?
Uchunguzi unaonesha kuwa miongoni mwa watu wengi
wanaosema hawawezi ni wale wenye kukosa hali ya uthubutu yaaani ni wale ambao
wao huogopa kufanya jambo fulani kisa tu wamejijengea imani kuwa hawawezi . Mafanikio
huja kwa kuziona fursa na kuzitumia sasa kwa kuwa hauna ule moyo wa uthubutu kila fursa inayokuja
wewe unasema huwezi na matokeo yake unaendelea kubaki pale pale bila kufanya
lolote zaidi unaendelea kujididimiza kwa kauli yako mbovu ya siwezi. Ki vipi unawezaje
kusema hauwezi ikiwa haujajalibu jambo husika? Umewezaje kujua kuwa hauwezi kwa
kukaa tu kuliangalia jambo bila kujihusisha nalo kisha ukasema aaa! Jambo hilo
siwezi. Nimesema kuwa watu wanaopenda kutumia kauli ya siwezi ni wale wenye
kukosa ile hali ya uthubutu yaani wao kwa namna yoyote ile huwa hawataki
kujaribu mambo, wao hukaa tu na kusema hawawezi.
Naamini wewe unayesoma makala hizi na kunufaika nazo
umeweza kufanya hivyo kwasababu ulithubutubu kujifunza kusoma na pengine
kuandika, ndio maana leo hii unauwezo wa kusoma makala hii na nyingine nyingi.
Sasa kama ulithubutu kujifunza kusoma na ukaweza na faida zake umeziona na
unaendelea kuziona, sasa kwanini leo hii
linapokuja suala la fursa fulani unagoma kuifuata kwa madai kwamba hauwezi. Nani
kakuambia huwezi?, Nani kakuaminisha kuwa hauwezi?, Unawezaje kusema hauwezi
ikiwa haujajaribu jambo husika?,. Ukijiuliza maswali haya na jibu likawa sijui.
Yaani hauna majibu ya ni nani alikuambia huwezi, uliamini vipi hauwezi ikiwa
hujajaribu basi jua fika unajidanganya na kujipotezea muda wako.
Jambo la msingi ambalo inabidi ulifahamu ni kuwa akili ya
mwanadamu hufanya kazi vizuri pale inapowekwa katika hali ya kufikiri juu ya
changamoto zinazokukabili. Akili yako huamka na kuchemka kufanya jambo pindi
unapojiuliza maswali kama kivipi ntafanya jambo hili, vile vile akili yako
hulala pale ambapo hauifanyi ikafikiri juu ya changamoto zinazokukabili na ndio
maana umekuwa bingwa wakauli za siwezi.
Acha mara moja
kutumia kauli ya siwezi hata kwa mambo ambayo hujajaribu, na hata kama
ulijaribu ukashindwa wafuate wale waliofanikiwa katika jambo husika ili uwaombe
ushauri pengine hautumii njia sahihi katika jambo husika ndio maana unashindwa.
Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
0754612413/0652612410.
No comments:
Post a Comment