Wednesday, December 2, 2015

Hii Sio Sababu Sahihi Ya Kutokufanikiwa Kwako.


Habari ya wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa mtandao ambao umejidhatiti katika kuhakikisaha unakupatia maarifa mapya, maarifa ambayo yatakufanya uwe bora na kuweza kuyafikia mafanikio makubwa sana maishani. Tumekutana tena katika kutaka kuelimishana juu ya mambo mbalimbali ambatana name ili ujue leo nimekuletea nini………
Ukizunguka mitaani ukawauliza vijana wengi wanaoshinda vijiweni wakipiga soga badala ya kufanya kazi kuwa kwanini wanafanya hivyo watakuambia hatuna kazi ya kufanya, ukiendelea  kuwauliza kuwa ,mbona kuna biashara nyingi, nanyi hamtaki kuzifanya? utasikia eeh! bwana eeh! hatuna mitaji. Hii ndio imekuwa kauli kubwa sana miongoni mwetu vijana,na hili ndilo lililonisukuma kuandaa makala hii pengine ulishawahi kukutana na kauli kama hii ya tatizo ni mtaji miongoni mwa vijana wengi au pengine nawe ni mojawapo ya watu wanaoitumia na kuiendekeza kauli hii ya tatizo ni mtaji.
Watanzania tumekuwa bendera fuata upepo, usinielewe vibaya  kwa kusema au kutumia kauli hii lakini haina budi kusema maana lazima tuwekane wazi maana ongezeko la kauli kuwa tatizo mtaji ni dhahiri kuwa ni jinsi gani vijana tumekosa fikira za kimapinduzi na badala yake tumekuwa vibendera fuata upepo ambapo ukisikia mwenzio kasema kuwa hajaanzisha jambo Fulani kwa sababu hana mtaji basi nawe unachukulia hivyo hivyo na kujivika sababu hiyo na kuifanya kuwa kama ngao kubwa ya kushindwa kwako katika biashara.
Kwanza jambo ambalo ni baya sana ambalo tumekuwan nalo na kwa kiasi kikubwa tumekuwa nalo ni kuamini kuwa pesa ndio mtaji muhimu katika biashara zetu, jambo hili ni imani potofu sana pamoja na kuwa tumeamini kuwa pesa ndio mtaji wa kwanza ambayo tayari ni imani potofu tuliyo nayo bado tumeendelea kujenga imani potofu juu ya imani potofu ambayo ni kuwa pamoja na kuamini kuwa pesa ndio mtaji nambari moja kwetu bado tumekuwa tukiamini kuwa ili kuanzisha biashara, ufugaji au shughuli za uwekezaji ama kilimo lazima tuwe na mitaji mikubwa yaani pesa nyingi. Leo hii sio ajabu kumkuta  kijana akitaka kuanzisha biashara fulani utakuta anapiga hesabu za mamilioni kama mtaji wakati anaweza kuanzisha biashara husika kwa mtaji hata wa laki moja.
Tabia ya kufikiria pesa nyingi katika uanzishaji wa biashara, kilimo au uwekezaji ndio kimekuwa chanzo kikubwa cha kuanza kwa kauli ya tatizo mtaji. Tumesahau kuwa hatua moja ndio huanzisha safari na ni hatua hiyo hiyo ndiyo umaliza safari ya umbali mrefu. Sio lazima uanze na pesa nyingi sana katika biashara yako au pesa nyingi katika uwekezaji wako. Nina mfano hai wa ndugu yangu ambaye alianza uwekezaji kwa mtaji wa shilingi 25,000, lakini leo hii anamiliki ekari za kutosha za mashamba ya miti ikiwa ni pamoja na usafiri wake binafsi( gari ya kutembelea). Yaani hapa ni rahisi sana kuuelezea mfano huu ni kuwa shilingi elfu 25 ndio iliyo zaa mamilioni. Kwahiyo ndio maana tunasema hatua moja ni muhimu kuliko hatua nyingi ulizotembea au utakazotembea. Kama mtu huyu angeogopa kutumia shilingi elfu 25 leo hii angebaki kulalamika kama wewe kuwa tatizo mtaji na wala leo nisingalimtumia kama mfano katika makala hii.
Ni kweli pesa kwa kiasi kikubwa ndio kila kitu katikashughuli za kilimo, biashara, uwekezaji na maeneo mengine ya kibiashara na kiuzalishaji lakini pesa pekee haitoshi. Je kama pesa pekee haitoshi nini basi kinatakiwa kitangulie kabla ya pesa?.
Kabla ya mtaji wa pesa kuanza mtaji nambari moja ni fikira au wazo/mawazo. Yaani huu ndio mtaji nambari moja ambao kila mtu anao leo hii huwezi kusema eti mtu fulani huwa hafikirii, yaani huo ni upotoshaji maana hakuna mtu ambaye huwa hafikirii. Kila mtu aliumbwa na uwezo huu wa kufikiri, na uwezo wa kufikiri unatofautiana toka kwa mtu hadi mtu na kinachofanya utofautiane ni namna ambayo kila mtu hutumia fikira zake katika kupambana na chagamoto zinazomkabili. Wale ambao hawataki kumiza bongo zao juu ya ni jinsi gani watakabiliana na changamoto za kimaisha ndio hukimbilia kusema pesa ndio mtaji na pamoja na kutambua kuwa pesa ni mtaji bado hao hao hurudi na kusema mtaji ambao ni pesa ni tatizo. Kila kitu huanza kama wazo kisha wazo hilo ndio hugeuzwa na kufanywa au kuleta pesa.  Kuna historia ya dada mmoja ambayo niliisoma katika kitabu fulani yeye alieleza kuwa hakuwa na pesa ya kuanzisha biashara aliyokuwa akiifikiria lakini alikuwa na wazo ambalo ndio mtaji wake, hivyo akashirikisha watu na baadae akapata pesa kwa ajili ya kuanzisha biashara yake hiyo. Mfano huu unatuonesha kuwa tatizo sio mtaji ambao unatufanya tushindwe kuanzisha biashara au shughuli za kilimo, au za uwekezaji bali mawazo yetu mabovu ndio hupelekea hali hiyo. Hivyo kwa kuwa wazo ndio mtaji mkubwa na mtaji huu ukiwa mbovu basi hatutaweza kufanya chochote zaidi ya kulaumu kuwa tatizo ni mtaji.
Usikae na kupiga piga makelele kijiweni kuwa tatizo ni mtaji bali kaa tulia na ufikiri utajikwamua vipi katika changamoto zinazokukabili na kumbuka matatizo hayatatuliwi kwa kukaa kijiweni na kupiga soga badala yake muda unaoutumia kupiga soga utumie katika kusoma vitabu au kufuatilia hadithi za watu waliofanikiwa wa ndani na nje ya nchi.
Ni mimi rafiki yako
Baraka Maganga

0754612413/0652612410.

No comments:

Post a Comment