Tuesday, December 1, 2015

Wafahamu Maadui Watano (5) Wa Mafanikio Yako.


Habari ya siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa. Ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya huku ukiwa mwenye hamasa na uliyejithatiti katika kuhakikisha kuwa unasonga mbele katika kuyatekeleza yale ambayo umekwisha kujiwekea kama malengo yako.
Leo tena tumekutana katika kuendelea kupeana mbinu na maarifa ambayo yatatufanya tuweze kuyafikia malengo yetu. Mara nyingi tumekuwa tukishindwa kutekeleza mipango yetu na pindi inapojitokeza hali hii huwa ni wepesi sana wa kuanza kutafuta sababu za kutokufanikiwa kwetu. Jambo baya ambalo tumekuwa tukilifanya ni kuangalia sababu za nje na kusahau sababu za ndani ambazo zimekuwa zikitupelekea kushindwa. Si ajabu kumkuta mtu kashindwa kwa ajili ya uvivu, uzembe, ukosefu wa hamasa kwake lakini anawageukia watu wengine na kuanza kuwashutumu kwa kushindwa kwake. Mara nyingi tabia hii ndio inayotufanya tusifanikiwe maana tunashindwa kugundua chanzo cha matatizo yetu ili tujirekebishe.  Hapa nakuletea maadui watano wa mafanikio yako kama ifuatavyo:-
1) Kuiga watu, kuna watu wanapenda sana kuwaiga wenzao. Kuiga au kumwiga mtu ni ile hali ya kuchukua au kufanya jambo kwa namna ambayo mtu mwingine anaifanya aidha kwa ruhusa(ridhaa) yake au kwa kuiba.Najua wapo watakao ona kuwa nikama nawadaganya hivi naposema kuiga ni adui wa mafaniko yao. Nasema kuiga ni adui wa mafanikio kwa kuzingatia msingi mmoja tu wa uigaji au aina moja ya uigaji ambayo ni ule uigaji wa kuiba. Huu ndio umekuwa ukifanywa na watu wengi yaani ukiona mtu fulani anafanya jambo fulani basi nawe unaanza kulifanya. Mfano umemwona mtu fulani anafanya biashara fulani basi nawe unaanza kuifanya biashara hiyo pengine kichwani mwako umemwiga biashara hiyo ili tu uweze kumwaribia yeye. Nitoe sababu iliyonifanya niseme kuiga ni adui wa mafanikio yako, kuiga kutakuwa adui wa mafanikio yako kwa sababu uigaji unaoufanya unakupunguzia wewe ubunifu na kukufanya usiwe mbunifu bali mtu ambaye anasubiri kutafuniwa alafu yeye ameze kiulaini. Chunguza leo hii, biashara, kazi za maofisini zinasuasua kwa kuwa zimejaa waigaji ambao ubunifu wamekosa kabisa. Chakufanya sasa kama umeyapenda mafanikio ya mtu kajifunze kutoka kwake mwombe akuelekeze hapo utapata vitu Vingi tofauti na pale ambapo wewe unataka uwe unamvizia tu nakufanya mambo yako kama yeye.
2) Kukosa uvumilivu,kabla hujafanikiwa utakumbana na changamoto kadha wa kadha. Safari ya mafanikio imejaa mabonde, mito, milima na vikwazo vya namna mbalimbali atakaye weza kupambana na vikwazo hivi ndiye atakaye yafikia mafanikio. Mafanikio yanahitaji mipango ya muda mrefu je? Upo tayari kuandaa mpango wa miaka kumi mpaka ishirini na kuhakikisha kuwa unakaa nao kwa miaka yote hiyo. Hapa sizungumzii uvumilivu wa muda mchache nazungumzia uvumilivu wa muda mrefu. Uvumilivu ni jambo gumu sana miongoni mwetu, wachache sana ambao wanaweza kuvumilia ndio maana leo hii wengi wamekuwa wakijidanganya kuwa mafanikio yana njia ya mkato jambo ambalo ni gumu sana tena sana. Katika mafanikio hakuna njia ya mkato bali uvumilivu unatakiwa sana tena sana ili kuweza kuyafikia mafanikio husika.
3) Kuambatana na makundi mabovu, makundi kila mtu anayo lakini wangapi tunauhakika kuwa makundi yetu sio mabovu. Kama unataka kujua kundi lako ni bovu au la angalia nini unapata kutoka katika kundi hilo. Je kundi linakusaidia wewe katika kutimiza ndoto yako au malengo yako. Kama jibu ni hapana kwa swali hilo basi jua kuwa kundi hilo ni bovu na halikufai lakini kama jibu ni ndio basi kundi hilo ni bora kwako na endelea nalo. Naposema kundi namaanisha watu ambao umekuwa ukishirikiana nao katika mambo yenu mbalimbali. Watu hawa waweza kuwa marafiki, ndugu au wanajamii wenzako wengine tu.
4) Kukosa mipango, maisha sio kuishi tu bali maisha ni kuishi kwa mipango, usiishi tu kwa kuwa kila ukiamka unaliona jua likichomoza basi unaridhika tu na hali hiyo pia ukiona giza limeanza kutanda unaona ni wakati wa kulala sasa. Hayo sio maisha, maisha ni pale utakapo jihoji na kupata majibu kuwa pale jua litakapo chomoza utafanya nini maana kila tulionapo jua ndipo tunajua kuwa ni siku nyingine sasa weka mipango kuwa kwa kila uitwao leo utafanya nini. Usiishi tu kwasababu kuishi kupo bali ishi kwa sababu unataka kuishi.
5) kukosa midhamu, nidhamu ni ule uwezo au Hali ya kuweza kupanga mambo yako na kuweza kuyasimamia pasipo kushindwa kuyasimamia. Yaani kama ulipanga kufanya jambo fulani alafu ukashindwa kwa sababu zako za uongo na kweli jua dhahiri hauna nidhamu. Mafanikio yanahitaji nidhamu katika kuyatekeleza Yale ambayo umekwisha kujiwekea usiweke tu mipango alafu ukashindwa kuitekeleza. Pindi utakapoweka mipango alafu ukashondwa kuitekeleza huo ni ukosefu wa nidhamu. Ukosefu wa nidhamu utakurudisha nyuma sana katika kuyaelekea mafanikio. Na wengi wetu hatufanikiwi kwa kuwa tumekosa nidhamu yaani hatuwezi kuisimamia mipango yetu ipasavyo.
Mafanikio hayana njia ya mkato na usipende kutafuta sababu za nje za kutokufanikiwa kwako bali chunguza sana mambo yako ya ndani ambayo ndio kikwazo cha mafanikio.
Ni Mimi rafiki yako.
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com
0754612413/0652612410.


No comments:

Post a Comment