Saturday, December 5, 2015

Hiki Ni Kitu Muhimu Sana Kuliko Unavyodhani.

Habari za wakati huu ndugu msomaji wa mtandao huu. Ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri na shughuli zako.Leo tena nakupa kitu kipya na kitu hicho ni umuhimu wa hatua moja. Je ulishawahi kufikiria umuhimu wa hatua moja? Basi endelea kusoma makala hii ili uweze kuufahamu umuhimu wa hatua moja.
Chukulia mfano ulikuwa unatembea kuelekea mahali usipo kujua katika kutembea huko ukafika sehemu ambapo kuna korongo kubwa sana ambapo ukitumbukia huko hakuna kupona na katika safari yako ilikuwa imebaki hatua moja tu ambayo ungeimalizia tu basi ulikuwa unatumbukia kwenye korongo hilo hivyo basi unamua kutokupiga ile hatua ya mwisho na hapo unakuwa umeokoa maisha yako.
Mfano mwingine, chukulia upo katika mashindano fulani ya mbio ambapo mshindi anapewa zawadi ya gari na nyumba. Ukaingia katika mashindano hayo huku ukiwa na uhakika na shauku ya kushinda hivyo ukaanza mbio hizo kwa kasi sana ukawaacha wapinzani mbali sana,lakini ghafla kabla ya kufika kwenye mstari wa mwisho ambapo ni hatua moja tu ili kufika mwisho ukaanguka vibaya sana na ikawa ngumu sana kwa wewe kuinuka, lakini kumbuka ni hatua moja tu ndio ilikuwa imebakia basi kwa kutambua hilo unajikakamua pamoja na maumivu yako unainuka na kumaliza mbio wa kwanza na hivyo kutangazwa mshindi na kujishindia zawadi. Jiulize ingekuwaje kama usinge jikakamua na kumalizia ile hatua moja.
Nimekuwekea mifano miwili ambapo mfano wa kwanza unaonesha umuhimu wa kupunguza hatua ili kuokoa maisha yetu. Inawezekana umekuwa ukifanya mambo mengi sana, sasa chagua jambo moja kati ya mambo mengi unayofanya na ulishikilie hilo mpaka ulikamilishe. Pia mfano huo unatuonesha na kutufunza kuwa ni muhimu tuyachunguze maisha yetu ili tuweze kubaini vikwazo vya ndoto zetu na tuvitoe.
Mfano wa pili unatuonesha kuwa tunaweza kukutana na vikwazo mbalimbali maishani ambavyo vinaweza kusababisha tusiyafikirie malengo yetu na hivyo kushindwa kabisa kuyatekeleza malengo yetu. Vikwazo hivyo ni kama kushindwa, kukata tamaa, hasara katika biashara, uvivu n.k. hivyo basi mfano huu unatuonesha kuwa pamoja na vikwazo vyote sisi tusonge mbele tu tusirudi nyuma kamwe.
Hatua moja ni muhimu iwe kwa kuiongeza au kuipunguza, hivyo jifunze wapi pa kuongeza hatua na ni wapi pa kupunguza. Maana hatua moja kati ya nyingi ndio huamua maisha yetu.
Ni Mimi rafiki yako,
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.
0754612413/0652612410.

posted from Bloggeroid

No comments:

Post a Comment