Habari ya siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya
maarifa ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri na
majukumu ya hapa na pale, yote haya ni
katika kuhakikisha kuwa unapata kuyatimiza yale ambayo umekwisha kuyaweka kama
malengo yako na mwisho wa siku unapata
mafanikio ambayo umekuwa ukiyatafuta kwa nguvu. Baada ya kuwa kimya kwa siku
mbili tatu hivi kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wangu, naomba
tureje na kuweza kuendelea kupeana maarifa ya hapa na pale.
Katika makala ya leo nataka kukushirikisha juu ya jambo
moja,Jambo lenyewe ni umuhimu wa kuanza kuheshimu vitu vidogovidogo. Nimeamua
kuandika juu ya jambo hili ili kuweza kukunasua katika mtego huu ambao unawaangamiza watu
wengi. Ndugu msomaji wa mtandao huu nataka nikusihi kwamba kwanzia leo jenga
tabia hii muhimu ambayo ni ya kuheshimu vitu vidogovidogo.
Nataka ujenge tabia hii kwa kuwa itakufanya ufanikiwe
zaidi. Kwanini jambo hili litakuifanya ufanikiwe ni kwa sababu vitu vidogo
ndivyo huwa vinavijenga vitu vikubwa. Chukulia mfano wa nyumba, nyumba haiwi
nyumba bila msingi sasa kwa hesabu za kawaida ukichukulia kigezo cha ukubwa
kimsingi,msingi wa nyumba ni mkubwa kuliko nyumba, lakini ukweli ni kwamba
nyumba haiwi nyumba bila msingi. Hivyo ili ujenge nyumba lazima uanze na msingi
bila msingi hakuna nyumba hivyo basi kwa kutumia mfano huu wa nyumba jenga
tabia ya kuvithamini vitu vidogovidogo.
Leo hii kuonesha ni jinsi gani watu hawathamini vitu
vidogo utamsikia mtu akikuambia siwezi kufanya biashara fulani kwa sababu nina
pesa chache ambayo haiwezi kunifanya nianzishe biashara hiyo husika, leo hii
watu wamekuwa wakisubiri kupata milioni kadhaa ndio waanzishe biashara zao hizo
wanazo zifikiria, lakini cha ajabu ni kuwa wamekuwa wakisubiri kwa miaka kadhaa
na wasipate hizo milioni za kuanzisha biashara zao husika. Kumbuka kuwa huwezi
kufika kumi bila kuanza na moja. Hivyo kama unataka kufika kumi lazima upitie
moja, mbili, tatu na kuendelea ndipo utafika kumi. Hivyo hata kama unataka
kufanya biashar ya mamilioni anza hata na maelfu yatakuwa na baadae itafika
hiyo milioni hakuna namna nyingine. Usiendelee kusubiri kupata milioni wakati
hauthamini pesa ndogo ambayo itakufanya ufike kwenye mamilioni.
Kudharau vitu vidogovidogo kumewaponza watu wengi sana na
kuwafanya wabaki pale pale na wasipige hatua yoyote ile ya kimaendeleo. Leo hii
watu hawawezi kujiwekea akiba ya pesa,kwa kuwa hawathamini pesa ndogondogo. Leo
hii mtu huona shilingi mia moja ni kama pesa ya kuchezea tu maana ni ndogo na
hawezi kuifanyia chochote. Kama unatabia hii acha mara moja maana itakugharimu
sio muda. Kuna msemo wa Kiswahili usemao “mazoea hujenga tabia”. Hivyo basi
kama huwezi kuthamini pesa ndogo kama shilingi mia uwapo na wazo la elfu kumi,vivyo
hivyo huto weza kuja kuithamini shilingi elfu kumi ukiwa na wazo la milioni,
hii ni kwa sababu usha jijengea tabia ya kuto kuthamini vitu vidogo huko nyuma.
Wapo watu ambao wamevithamini vitu vidogo na matokeo yake
wakapata mafanikio makubwa, kuna mifano ya watu ambao waliamua kuanzisha
biashara zao wakiwa na mitaji midogo sana ambayo hata wakikuambia leo hii
utawaona kama waongo wenye lengo la kukudanganya tu, lakini ukweli ni kuwa watu
hawa walielewa umuhimu wa kuvithamini vitu vidogo ndio maana wakaamua kuanzisha
biashara zao japo kuwa walikuwa na mitaji midogo na matokeo yake ni kuwa
walifanikiwa sana maishani mwao, hivyo jifunze kupitia watu hao ambao
wamefanikiwa.
Kama kweli unataka kufanikiwa basi jenga tabia ya
kuvithamini vitu vidogo maana hivyo ndivyo huleta mafananikio makubwa kumbuka
mfano wa punje moja ya mhindi ambayo hufukiwa ardhini na baadae huzaa punje
nyingi ambazo hutumika kama chakula cha kuwasaidia watu.
Ni mimi rafiki yako
Baraka Maganga.
0754612413/0652612410.
No comments:
Post a Comment