Monday, November 23, 2015

Kitu Hiki Kimoja Kinatushinda Wengi Na Kuturudisha Nyuma.


Habari za Siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa, mtandao ambao umejidhatiti katika kuhakikisha unakupa maarifa mapya kila Siku na kukusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha maisha yako na kuifanya safari yako ya kuelekea mafanikio isiwe ya kukuchosha na kukatisha taama. Ambatana nami katika makala ya leo ili ujue leo nimekuletea kitu gani kipya.



Mara nyingi sana binadamu tumekuwa ni watu wa kupanga mambo mengi sana juu ya maisha yetu, tumekuwa ni mabwana mipango, na wengi tumekuwa wenye kuweka mipango mingi sana lakini shida inakuja pale ambapo inatupasa tutekeleze hiyo mipango yetu. Asilimia kubwa sana ya watu tumekuwa wenye kuweka mipango mingi na malengo mengi yasiyotekelezeka yaani wengi wetu mipango yetu na malengo yetu hubaki vichwani mwetu au katika karatasi za daftari ambamo huwa tunakuwa tumeandika na kuhifadhi mipango na malengo yetu hayo. Tumekuwa ni kina bwana panga pangua hii ni kutokana na sababu kuwa tumekuwa tukiweka mipango hii na malengo yale lakini ghafla tunaivunja na kuweka mipango mingine mipya. Huu umekuwa mchezo wa tulio wengi sana. Je? Unajua nini kinatufanya tuwe hivyo. Kama haujui basi ambtana nami. Kuna sababu moja kuu ambayo imekuwa ikifanya hali hii itokee nayo ni kushindwa  kujitoa kisawasawa.
Utekelezaji wa mipango na malengo yetu vinahitaji kujitoa kisawasawa, kupanga malengo yetu na mipango yetu kisha kuiandika katika vijitabu vyetu vya kumbukumbu zetu haitoshi kutufanya au kutuonesha wenye mafanikio. Ili utekeleze mipango yako na malengo yako ni lazima ujitoe kweli. Kuandika malengo au kupanga mipango yako hakukufanyi uwe mwenye mafanikio bali utekelezaji wa mipango na malengo husika ndio hutuletea mafanikio.
Baada ya kuwa umepanga malengo na mipango yako na ukaamua kuitekeleza kisawasawa, ukaanza kuifanyia kazi mipango hiyo lakini kila unapojaribu kuitekeleza mipango hiyo unajikuta umeshindwa kuitekeleza, unajaribu tena kwa Mara ya pili unashindwa, unajaribu tena na tena lakini matokeo yanabaki vile vile. Unajua kwanini hali hii inajitokeza?
Hali hii inajitokeza kwa kuwa ndio umepanga mipango na malengo yako vizuri lakini hujajitoa kikamilifu katika kuhakikisha unayatimiza Yale uliyoyapanga, ndio hujajitoa kisawasa pengine unasema hapana Mimi mbona najituma katika shughuli zangu nafanya hivi na vile ili kutekeleza yale niliyojiwekea na kujipangia lakini sipati matokeo mazuri kwanini inakuwa hivi. Jibu ni kuwa hujajitoa kisawasawa.
Unaweza kujiona umejitoa kisawasawa katika kutekeleza mipango na malengo yako lakini kumbe ndani ya kule kujitoa kwako kumeambatana na hali ya uvivu hivyo ule uvivu unakufanya usifanye kazi kwa kiwango kile kinachotakiwa ili kukuwezesha kuyatekeleza Yale malengo yako. Ikiwa unafanya shughuli zako na unajiona kuwa unaweka jitihada za kutosha kuyatekeleza Yale uliyojipangia lakini matokeo yanakuja tofauti na ulivyotegema jua kuwa hujajitoa kisawasawa, kunasehemu ambayo unafanya shughuli kivivu na ndio maana unashindwa kupata matokeo mazuri.
Endapo utapanga mipango yako vizuri na ukajitoa kisawasawa basi nakuhakikishia kuwa utafanikiwa kwa kiasi kikubwa hakuna jambo ambalo litakufanya usipate matokeo Yale ambayo uliyategemea, maana kujitoa kutakusaidia wewe kuondokana na hali ya uvivu, kukata tamaa na visingizio vya hapa na pale.
Unapoweka mipango na malengo yako hakikisha umejitoa kisawasawa katika kuyatekeleza usiweke tu mipango kisha ukaacha tu mipango inaelea elea, na utambue kuwa mipango haiwezi kujitekeleza yenyewe.
Ni Mimi rafiki yako.
Baraka Maganga.
Bmaganga22@gmail.com.

0754612413/0652612410.

2 comments: