Thursday, December 31, 2015

Hii Ni Silaha Mojawapo Ya Watu Waliofanikiwa.


Habari za leo mpendwa msomaji wa mtandao huu wa kona ya maarifa ni matumaini yangu kuwa hu mzima wa afya na unaendelea vizuri katika kuhakikisha kuwa unaupokea mwaka mpya vizuri ikizingatiwa kuwa tumebakiza masaa sasa kuukamilisha mwaka 2015 na kuingia mwaka mpya wa 2016. Basi katika kumaliza mwaka nataka umalize na wazo hili ili ukalitumie vizuri mnamo mwaka wa 2016 na kuendelea.
Je unazijua silaha muhimu za watu waliofanikiwa?, pengine unazijua baadhi kama vile kujiamini, kujituma, kujiwekea malengo, uwajibikaji, kushirikiana na timu sahihi n.k. hizo ni baadhi kati ya silaha nyingi ambazo waweza kuwa unazijua, lakini leo nakupatia silaha moja muhimu sana ya watu waliofanikiwa na kwa kuwa nawe unataka kufanikiwa ichukue na uitumie silaha hii ipasavyo.Matumizi sahihi ya muda, hii ndio silaha muhimu ya watu waliofanikiwa na kama nawe kweli unataka kufanikiwa hakikisha unaichukua silaha hii na kuitumia katika safari yako. Watu waliofanikiwa wanajua kutumia muda ipasavyo, wanajua kuwa kwa kila siku tuna masaa ishirini na nne (24) na katika hayo masaa kuna muda wa uzalishaji na muda usio zalishi (uzalishaji). Kwa kutambua hilo uhakikisha kuwa hawapotezi muda ovyo.
Watu waliofanikiwa wanatumia muda wao mwingi sana katika shughuli zao na sio katika starehe wala kupumzika, au kuangalia televisheni. Hii ni kwa kuwa wanatambua kuwa kuna muda wa uzalishaji na muda usio zalishi na kwa kuwa wanalitambua hilo basi wao hutumia muda vizuri katika shughuli zao yaani kama ana biashara basi muda mwingi sana atautumia katika biashara yake na sio kukaa kijiweni kupiga stori. Na kama ni mwekezaji basi muda wake mwingi atautumia katika shughuli zake za kiuwekezaji.
Watu waliofanikiwa wanatumia muda wao vizuri kwa kuwa wanajua kuwa muda ni mali ya kipekee ambayo ukiipoteza huwezi kuitafuta na kuipata tena yaani wao wanafalsafa ya kuwa muda ni kitu cha kipekee kisichoweza kurudishwa. Kama kweli unataka kufanikiwa naomba ujenge picha hii akilini mwako ili ukusaidie kuutumia muda wako vizuri. Ufananishe muda wako sawa na mafuta katika gari, mafuta katika gari ni kitu cha muhimu sana maana bila mafuta gari haliwezi kwenda popote, lakini mafuta haya huwa hayana kuongezeka bali ni kupungua tu na hatimaye kuisha ambapo ukitaka gari liendelee kwenda inabidi ukatafute mengine (kununua), uweke ndipo gari liendeleee na safari zake. Ndivyo ulivyo muda kama ambavyo hakuna nyongeza ya mafuta katika tenki la gari basi hata muda ni hivyo hivyo yaani tuna masaa ishirini na nne kwa siku moja basi hakuna pungufu wala nyongeza ya hapo. Hivyo basi inabidi ujifunze kufanya shughuli zako ipasavyo kulingana na muda  husika uliopewa.
Muda ni kitu ambacho kimekuwa kikidharauliwa na watanzania wengi sana tena sana na kwangu mimi matumizi mabovu ya muda ni sababu moja wapo ya watu wengi kutofanikiwa maishani. Watanzania wengi sana tumekuwa na tatizo ya kutojua kutumia muda na ndio maana hatuuthamini. Hauwezi kukithamini kitu bila kujua umuhimu wake, leo nataka utambue kuwa muda ni kitu muhimu sana tena sana na kwanzia sasa anza kuuthamini muda maana muda unaweza kuwa kigezo cha kutofautisha mafanikio na kushindwa.
Dunia imebadilika na itaendelea kubadilika na kubadilika, maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta vitu vingi sana vya kukuibia muda usipokuwa makini utajikuta kila siku ukiwauzia watu wengine muda bila wewe kunufaika na chochote bali kuwanufaisha wengine, zinduka wewe ukiyekatika usingizi mzito, acha kupoteza muda wako ovyo kwani muda ni rasilimali muhimu kwako ambayo ni ya bure kabisa kwako.
Ni mimi rafiki yako,
Baraka Maganga
Wasiliana nami kwa.
Simu: 0754612413 au 0652612410.
Barua pepe: Bmaganga22@gmail.com.


No comments:

Post a Comment